Yaliyojiri Viwanja: Yote Unayotakiwa Kujua Kuhusu Ligi Za Ulaya Wikiendi Iliyopita

7th October 2019

MANCHESTER, Uingereza -Ligi kuu za nchi mbalimbali barani ulaya zimeendelea wikiendi hii iliyopita ambapo mambo mengi yamejitokeza kama yalivyokusanywa na dawati la SportPesa News.

Daniel James
Daniel James
SUMMARY

Kama hali itaendelea hivi baada ya mapumziko kupisha timu za taifa, nadhani hali itakuwa ngumu zaidi kwa kocha huyo raia wa Norway kuendelea kubaki Old Trafford.

Manchester United, Tottenham Hali Tete

Hali inazidi kuwa mbaya kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United baada ya kukubali kipigo kingine cha fedheha mbele ya Newcastle United walioibuka na ushindi wa 1-0.

Kipigo hicho kwa Man United ni cha tatu msimu huu wakiwa wameshuka dimbani mara nane na sasa wamebaki kwenye nafasi ya 12 kwenye msimamo wakiwa na alama 9 mbili juu ya mstari wa kushuka daraja.

Kama hali itaendelea hivi baada ya mapumziko kupisha timu za taifa, nadhani hali itakuwa ngumu zaidi kwa kocha huyo raia wa Norway kuendelea kubaki Old Trafford.

Nao Tottenham Hotspurs wamwezidi kujiweka kwenye mazingira magumu baada ya kufungwa tena kwa mabao 3-0 dhidi ya Brighton kwenye mchezo wa ligi kuu.

Hiyo imekuja siku chache baada ya timu hiyo kulambwa mabao 7-2 na Bayern Munich kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa.

Eden Hazard Ameanza Maisha Mapya

Baada ya kuanza maisha kwa kusuasua ndani ya Real Madrid, hatimaye winga mpya wa klabu hiyo aliyesajiliwa kwa pesa ndefu kutoka Chelsea ameanza kuonesha cheche baada ya kufunga bao moja kwenye ushindi wa 4-2 dhidi ya Granada.

Ushindi huo umewabikisha Madrid kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na alama 18 baada ya kushuka dimbani mara nane msimu huu. Mabao mengine ya Madrid kwenye mchezo huo yamefungwa na James Rodriguez, Luka Modrick na Karim Benzema.

Juventus Wamekalia Usukani

Gonzalo Higuain amefunga bao muhimu la ushindi lililoisaidia timu yake ya Juventus kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Inter Milan kwenye uwanja wa San Siro. 

Ushindi huo umeifanya Juventus kukalia kileleni kwenye msimamo wa Serie A kwa mara ya kwanza msimu huu wakiwaondoa Milan ambao walianza ligi hiyo kwa kishindo.

Bao lingine la Juventus kwenye mchezo wa jana limefungwa na Paul Dyabala huku la kufutia machozi la Milan likifungwa na Lautaro Martinez.

Bayern Munich Wametakaswa

Baada ya kuibuka na ushindi mnene wa mabao 7-2 kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa ugenini dhidi ya Tottenham, siku ya Jumamosi klabu ya Bayern Munich imejikuta ikiangukia pua kwenye uwanja wao wa nyumbani baada ya kufungwa kwa 2-1 dhidi ya Hoffenheim.

Hata hivyo kipigo hicho bado hakijawatoa kileleni kwani sasa wanalingana pointi na Freiburg wote wakiwa na alama 14 baada ya kucheza mechi saba.

Barcelona Wachachamaa

Licha ya wachezaji wawili kutolewa kwa kuoneshwa kadi nyekundu lakini klabu ya Barcelona wameonesha ukomavu wa hali ya juu na kuondoka na pointi tatu muhimu baada ya kushinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Sevilla.

Mabao kwenye mchezo huo yamefungwa na Luis Suarez, Arturo Vidal, Osmane Dembele na Lionel Messi huku Dembele na Ronald Araujo wakioneshwa kadi nyekundu kwa upande wa Barcelona.

Ushindi huo unawapeleka Barcelona hadi kwenye nafasi ya pili ya msimamo wakiwa na alama 16 mbili nyuma ya vinara Real Madrid.

Tammy Abraham Hakamatiki

Akiwa na umri wa miaka 19 tu, kinda wa Chelsea, Tammy Abraham amezidi kuonesha makali yake baada ya kufunga bao lingine na kufikisha idadi ya mabao 8 sawa na Kun Aguero ambaye ni kinara wa ufungaji.

Abraham alifunga bao la kwanza wakati Chelsea wakishinda mabao 4-0 ugenini dhidi ya Southampton, mabao mengine kwenye mchezo huo yamefungwa na Mason Mount, Ngolo Kante na Mitchy Batshuay.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya