Yaliyojiri Kwenye Michuano Ya Kombe La Dunia Rugby Japan

7th October 2019

TOKYO, Japan -Michuano ya kombe dunia ya Rugby inaendelea kwa kasi nchini Japan wakati miamba wakiendelea kutoana jasho kwenye viwanja mbalimbali.

Rugby
Rugby
SUMMARY


Kwenye kambi ya timu ya taifa ya Uingereza hali si shwari wakati wakijiandaa kukabiliana na Ufaransa siku ya Jumamosi baada ya mchezaji wao tegemeo Billy Vunipola kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

Dawati la SportPesa News linakuletea baadhi ya matukio muhimu yaliyojitokeza na yanayotarajia kujitokeza kwa siku za usoni

Wenyeji Japan Watakata

Wenyeji wa michuano ya Rugby kombe la dunia nchi ya Japan wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuwafunga Samoa kwa jumla ya alama 38-19.

Ushindi huo unawafanya wenyeji hao kukalia usukuani wa kundi A ambalo pia lina timu za Ireland, Scotland na Urusi. 

Japan sasa watacheza na Scotland siku ya Jumatano kwenye mchezo wa mwisho wa kundi hilo na kama watafanikiwa kuibuka na ushindi basi watakuwa wametinga robo fainali ambapo watakutana na timu iliyoshika nafasi ya pili kwenye kundi B ambapo kuna timu za New Zealand, Italia, Namibia na Afrika Kusini.

Rungu Latembezwa Kwa Watovu Wa Nidhamu

Mchezaji wa Argentina, Tomas Lavanini amefungiwa mechi nne baada ya kuonesha mchezo mbaya dhidi ya nahodha wa Uingereza Owen Farrell.

Tukio hilo limetokea kwenye mchezo uliofanyika juzi usiku ambapo Uingereza waliichakaza Argentina kwa jumla ya alama 39-10.

Mbali na mchezaji huyo, pia nahodha wa Italia, Andrea Lovotti na Nicola Qauglio wamefungiwa mechi tatu kwa mchezo mbaya walioonesha dhidi ya wachezaji wa Afrika Kusini.

Kwenye mchezo huo, Afrika Kusini waliwafunga Italia waliokuwa pungufu ya wachezaji wawili uwanjani kwa jumla ya alama 49-3.

Uingereza Tumbo Joto

Kwenye kambi ya timu ya taifa ya Uingereza hali si shwari wakati wakijiandaa kukabiliana na Ufaransa siku ya Jumamosi baada ya mchezaji wao tegemeo Billy Vunipola kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

Vunipola alishindwa kuendelea na mchezo wakati Uingereza ikapata ushindi wa 39-10 mbele ya Argentina siku ya Jumamosi.

Taarifa zinaeleza kuwa kocha msaidizi wa Uingereza, Neal Hatley amesema kuwa hawatamuhatarisha Vunipola kwa kumchezesha siku ya Jumamosi na badala yake sasa wanamuandaa Mark Wilson kuziba nafasi hiyo.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya