Wales, Hungary Uso Kwa Uso Kuamua Nani Afuzu Euro 2020

19th November 2019

CARDIFF, Wales- Leo kwenye dimba la Cardiff nchini Wales itapigwa mechi moja ya kukata na shoka ambayo itatoa majibu timu ipi ifuzu michuano ya Euro mwakani

Gareth Bale
Gareth Bale
SUMMARY

Ushindi wowote kwa Wales ambao wanafundishwa na Ryan Giggs utawafanya kufuzu kucheza Euro moja kwa moja kwa mara ya pili mfululizo.

Mechi hiyo ni kati ya timu ya taifa ya Wales ambao watakuwa ni wenyeji kuwakaribisha Hungary.

Ugumu na umuhimu wa mechi hiyo kwa timu zote mbili unasababishwa na nafasi walizokuwa nazo kwenye msimamo. Hungary ambao leo wapo ugenini wanakalia nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na alama 12.

Wales ambao ni wenyeji wa mechi ya leo wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 11 kwenye msimamo.

Ushindi wowote kwa Wales ambao wanafundishwa na Ryan Giggs utawafanya kufuzu kucheza Euro moja kwa moja kwa mara ya pili mfululizo.

Kama unadhani utata umeisha ndani ya mechi hiyo basi hapana unajidanganya. Kuna timu inaitwa Slovakia yenyewe ipo nafasi ya nne ikiwa na alama zake 10 na endapo mechi kati ya Wales dhidi ya Hungary ikiisha sare itakuwa faida kwao.

Kwanini? Mechi hiyo ikiisha kwa sare itakuwa faida kwa Slovakia endapo wao watapata ushindi kwenye mchezo wao wa leo dhidi ya Azerbaijan ambao ni vibonde wa kundi.

Wakishinda watafikisha alama 13 ambazo bila shaka zitakuwa sawa na Hungary na hapo ndipo itakuwa faida kwao kwasababu timu hizo mbili zilipokutana Slovakia aliweza kuwafunga Hungary.

Kwahiyo kwa kifupi ni kwamba timu tatu zina uwezo wa kukamata nafasi ya pili baada ya mechi za leo usiku. Nafasi ya kwanza tayari ilishanyakuliwa na Croatia ambaye yeye alifuzu mapema kabisa.

Kwenye kikosi cha Wales leo watakuwa na furaha ya kuwapokea kikosini Gareth Bale na Aaron Ramsey ambao walikuwa ni majeruhi kwenye michezo iliyopita.

Bwana mdogo Daniel James anayecheza Manchester United anatarajiwa kama kawaida kuwasha moto wake akitokea upande wake wa kushoto mwa uwanja.

Kukamilisha Ratiba

Mbali na pambano hilo la kukata na shoka leo, mechi nyingine nyingi za leo zitakuwa ni za kukamilisha ratiba. 

Uholanzi, Ujerumani na Ubelgiji ni miongoni mwa timu ambazo leo zinacheza lakini tayari zilikuwa zimeshafuzu tangu wiki iliyopita na wengine wakifuzu tangu mwezi uliopita.

Ratiba Kamili

Ujerumani vs Northern Ireland

Wales vs Hungary

Scotland vs Kazakhstan

Uholanzi vs Estonia

Slovakia vs Azerbaijan

Latvia vs Austria

North Macedonia vs Israel

Poland vs Slovenia

San Marino vs Urusi

Ubelgiji v Cyprus

Imeandaliwa na Jerry Mlosa