Ushindi Dhidi Ya Coastal Union Wampa 'Jeuri' Mkwasa

18th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa amesema ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union jana kwenye mchezo wa kirafiki ni matokeo ya kile ambacho wamekuwa wakikifanyia kazi mazoezini tangu alipopewa timu.

Charles Boniface Mkwasa
Charles Boniface Mkwasa
SUMMARY

Mkwasa ana kaimu nafasi ya kocha mkuu wa Yanga akichukuwa kijiti kilichoachwa na kocha Mwinyi Zahera ambaye alitimuliwa kazi mapema wiki iliyopita.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo uliopigwa uwanja wa Taifa, Mkwasa amesema wachezaji wake waliweza kutekeleza kile alichowaelekeza licha ya changamoto kujitokeza kwenye umaliziaji hasa kipindi cha kwanza.

"Tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi kwenye kipindi cha kwanza lakini washambuliaji wangu hawakuwa wakijipanga vizuri hivyo kupoteza nafasi hizo"

"Tulikuwa imara katika ulinzi ndio maana umeona hata bao walilofunga Coastal Union lilikuwa la mchezaji wetu kujifunga. Tuliwabana wakashindwa kutengeneza nafasi za wazi"

"Kipindi cha pili niliwaambia wachezaji wangu waongeze presha langoni kwa Coastal Union, tulitengeneza nafasi nyingi baadhi tumeweza kuzitumia," amesema Mkwasa.

Aidha Mkwasa amesema bado kazi kukiimarisha kikosi chake inaendelea lakini anaridhishwa na mwenendo wa timu mpaka sasa.

Kwenye mchezo wa jana wa kirafiki Coastal Union walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia mlinzi wa Yanga, Ally Mtoni ambaye alijifunga wakati akijaribu kuokoa hatari langoni kwake.

Hata hivyo Yanga waliamka kipindi cha pili na kufunga mabao matatu kupitia kwa Mrisho Ngassa, Papy Tshishimbi na Juma Balinya huku David Molinga akikosa penati kwenye mchezo huo.

Mkwasa ana kaimu nafasi ya kocha mkuu wa Yanga akichukuwa kijiti kilichoachwa na kocha Mwinyi Zahera ambaye alitimuliwa kazi mapema wiki iliyopita.

Yanga wanajiandaa na mchezo ujao wa ligi kuu bara dhidi ya JKT Tanzania uliopangwa kufanyika mara tu baada ya ratiba ya mechi za kimataifa kuisha.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya