Uchambuzi: Makocha 5 Wenye Nafasi Ya Kurithi Kibarua Cha Unai Emery Arsenal

30th November 2019

LONDON, Uingereza- Baada ya klabu ya Arsenal kuamua kuachana na kocha Unai Emery aliyedumu kwenye timu hiyo kwa miezi 18. Habari sasa zimegeukia upande wa kutafuta warithi ambao watakaoshika nafasi ndani ya timu hiyo.

Nuno Espirito
Nuno Espirito
SUMMARY

Mreno huyu alipanda daraja na timu hiyo msimu uliopita na alifanikiwa kufanya mambo makubwa yaliyowezesha timu hiyo kushika nafasi ya saba na kukata tiketi ya Europa msimu huu.

Majina mengi yamekuwa yakitajwa na vyombo mbalimbali vya habari duniani kote ambapo mtandao wa SportPesa News unakusogezea majina matano yenye nafasi kubwa zaidi.

Nuno Espirito Santo (Wolves)

Kwasasa kocha huyu anakiongoza kikosi cha Wolves kinachoshiriki michuano ya ligi kuu ya Uingereza pamoja na ligi ya Europa.

Mreno huyu alipanda daraja na timu hiyo msimu uliopita na alifanikiwa kufanya mambo makubwa yaliyowezesha timu hiyo kushika nafasi ya saba na kukata tiketi ya Europa msimu huu.

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vinaeleza kuwa mazungumzo baina ya mabosi na wawakilishi wa kocha huyo yameshaanza na kocha mwenyewe anavutiwa zaidi na kazi hiyo ya kukinoa kikosi cha Arsenal.

Kazi itakuwa ni kwa mabosi wa Arsenal kuweza kukubaliana na kocha huyo pamoja na Wolves kwa ajili ya kuvunja mkataba.

Mauricio Pochettino

Hili ni jina maarufu na huenda mashabiki wengi wa Arsenal wanatamani kumuona kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs akishika kijiti ndani ya timu yao.

Amedumu Spurs kwa miaka mitano hadi alipotimuliwa kazi wiki iliyopita baada ya kufanikiwa kuiongoza timu hiyo hadi fainali ya ligi ya mabingwa msimu ulipiata.

Hakuwa na mafanikio makubwa ya kubeba mataji lakini aina ya soka lake na jinsi anavyoamini zaidi vijana kwenye timu anazofundisha huenda ikawa moja ya sababu zitakazoweza kumpa kazi.

Kumpata kwake siyo kazi kama Nuno kwasababu yeye hana mkataba na timu yeyote na hivyo ni mazungumzo tu ya mkataba wake ingawa kuna tetesi kuwa pengine anaweza kuelekea Bayern Munich.

Max Allegri 

Kama ilivyo kwa Pochettino, Max Allegri naye ni kocha mkubwa ambaye hana timu anayofundisha kwasasa.

Kocha huyo aliondoka Juventus baada ya kumalizika kwa msimu uliopita ambapo alidumu kwenye timu hiyo kwa miaka mitano na kushinda mataji ya Serie A kwenye kipindi chake chote cha uongozi.

Tetesi za awali zilikuwa zikimtaja kuhusishwa zaidi na Manchester United lakini mabosi wa Arsenal wanaaminika kumuingiza kweney orodha yao ya makocha wanao wahitaji kuziba nafasi ya Unai.

Hata hivyo bado haijafahamika kama kocha huyo atakubaliana na kazi hiyo ya kwenda kujenga timu au atasubiri kazi ya timu ambayo ipo tayari kwa mapambano.

Mikel Arteta (Man City)

Kiungo wa zamani wa Everton na Arsenal kwasasa anafanya kazi ya kumsaidia kocha Pep Guardiola ndani ya Manchester City.

Mabosi wa Arsenal wanaamini kuwa ujuzi aliopata kijana huyo chini ya kocha Guardiola kwa kipindi cha miaka mitatu inaweza ikawa faida kwao kwa kukiendeleza kikosi chao.

Pia Arteta anaonekana kuwa ni mtu ambaye anakijua zaidi kikosi cha Arsenal ukilinganisha na makocha hao wote watatu ambao nimewataja hapo juu.

Hata hivyo haitakuwa kazi rahisi kumng'oa hapo kwani tayari kocha Guardiola alishaanza kuzipiga mkwara timu zinazomtaka wakiwemo Everton ambao nao wanahatihati ya kutimua kocha siku za usoni.

Freddie Ljungberg

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Arsenal ambaye alirejea Arsenal msimu uliopita kama kocha msaidizi chini ya Unai Emery.

Kwasasa Ljungberg ndiye amekabidhiwa mikoba hiyo kwa muda akisubiri hatma ya kutangazwa kocha mkuu lakini habari za ndani zinabainisha kuwa na yeye yumo kwenye orodha ya watakao hojiwa ili kuchukuwa nafasi ya kocha wa kudumu.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya