Uchambuzi: Hizi Hapa Mechi 6 Bab Kubwa Za Mwinyi Zahera Ndani Ya Yanga

6th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Siku moja imepita tangu uongozi wa Yanga ulipotangaza kuachana na Mwinyi Zahera ambaye alihudumu kama kocha wa timu hiyo kwa takribani msimu mmoja na nusu.

Mwinyi Zahera
Mwinyi Zahera
SUMMARY

Timu ya Pyramids haina historia kubwa kwenye soka la Afrika na mashabiki wengi wa Yanga waliofurika uwanja wa CCM Kirumba walitegema kuona timu ikipata matokeo chanya ya kujiweka pazuri ili kutinga hatua ya makundi.

Hata hivyo hali haikuwa kama walivyodhania kwani walipigiwa mpira mwingi na kufungwa kwa 2-1 kitu kilichoibua hasira kwa umati wa wana Yanga.

Siyo Zahera tu bali benchi zima la ufundi kuanzia kwa kocha msaidizi Noel Mwandila limefutwa na sasa Yanga wamemtangaza Charles Boniface Mkwasa kuwa kocha wa muda hadi pale watakapompata kocha mkuu wakudumu.

Zahera alijiunga Yanga mwishoni wa msimu wa 2017-18akichukuwa nafasi iliyoachwa wazi na George Lwandamina. 

Hata hivyo kazi yake rasmi aliianza mwanzoni mwa msimu wa 2018-19 kutokana na matatizo ya vibali ambayo yalimsababishia kuangalia mechi nyingi akiwa jukwaani huku timu ikiogozwa na Mwandila.

SportPesa News inakuleta mechi sita za kukumbukwa zaidi kwenye kipindi chote ambacho Zahera alikuwa kocha wa Yanga.

Yanga 2-1 USM Alger

Mechi hii ilichezwa Agosti 19, 2018 ndani ya dimba la taifa. Naweza kusema ndiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha Mwinyi Zahera kuiongoza timu yake akiwa kwenye benchi la ufundi.

Huu ulikuwa ni mchezo wa hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika. Na mchezo huu ulikuwa ni watano kwa Yanga. Kwenye michezo yao minne iliyopita walikuwa hawajapa ushindi hata kwenye mechi moja.

Mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa 2-1 mabao ya Deus Kaseke na Heritier Makambo.

Kutokana na aina ya timu waliyoifunga, mashabiki wengi wa Yanga walijenga imani kubwa sana na Zahera na walikubali uwezo wake siku ya kwanza tu baada ya kukalia benchi.

Yanga 0-0 Simba 

Mchezo wa watani wa jadi uliochezwa Septemba 30, 2018 ndani ya dimba la taifa. Mchezo huu ulikuja haraka kwenye mechi za mwanzo wa msimu wakati Yanga wakiwa wameanza ligi kwa kasi kubwa wakiwa wameshinda mechi zao nne za awali.

Hata hivyo licha ya imani kubwa waliyokuwa nayo kuelekea mchezo huo walijikuta kwenye wakati mgumu sana siku ya mchezo kwani Simba walitawala kwa zaidi ya asilimia 70.

Walifanya mashambulizi mfululizo na kama si uwepo wa kipa Beno Kakolanya kwa siku ile pengine Yanga wangeandika rekodi mbaya sana mbele ya watani zao wa jadi.  

Stand United 1-0 Yanga

Baada ya kucheza takribani michezo 19 bila kufungwa, hatimaye ilipofika Januari 19, 2019, Yanga walikubali kipigo cha kwanza cha msimu cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United.

Bao la Stand lilifungwa dakika ya 88 na Jacob Masawe kipindi ambacho watu wengi walishaamini kwamba huenda mchezo huo ungeisha kwa sare ya bila kufungana.

Kumbuka kuwa kwenye msimu huo uliopita Yanga walipata tabu sana mbele ya Stand United ambapo kwenye mchezo wao wa kwanza licha ya kuibuka na ushindi wa 4-3 lakini walishuhudia Alex Kitege akiwapiga Hat Trick.

Lipuli 1-0 Yanga

Mechi hii ya Machi 16, 2019 ilikuwa ni mechi ya tatu kwa Yanga kufungwa msimu huo wa 2018-19.

Lipuli waliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Haruna Shamte. Kitu ambacho kinafanya mechi hii isisahaulike ni ule uamuzi wa Zahera kuamua kubaki Dar es salaam kuwapokea AS Vita ya Congo waliokuja kucheza na Simba wakati huo timu yake ikielekea Iringa.

Township Rollers 0-1 Yanga

Baada ya kutoka sare ya 1-1 kwenye uwanja wa taifa watu wengi waliamini Yanga safari yao kwenye ligi ya mabingwa ilikuwa imefika mwisho. 

Hata hivyo Agosti 24, 2019 nchini Botswana bao la Juma Balinya lilibadili hali yote ya mchezo na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi muhimu wa bao 1-0 ugenini, ushindi ambao uliwafanya kusonga mbele na kukutana na Zesco United.

Yanga 1-2 Pyramids

Kama utakuwa ni mfuatiliaji mzuri wa mambo unaweza ukajua tu kwamba tatizo hadi kutimuliwa kwa Zahera lilianzia hapa.

Oktoba 27, 2019 Yanga walikuwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba wakiutumia kama uwanja wa nyumbani kuwakaribisha waarabu wa Misri, Pyramids kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika hatua ya mtoano.

Timu ya Pyramids haina historia kubwa kwenye soka la Afrika na mashabiki wengi wa Yanga waliofurika uwanja wa CCM Kirumba walitegema kuona timu ikipata matokeo chanya ya kujiweka pazuri ili kutinga hatua ya makundi.

Hata hivyo hali haikuwa kama walivyodhania kwani walipigiwa mpira mwingi na kufungwa kwa 2-1 kitu kilichoibua hasira kwa umati wa wana Yanga.

Wapo walioanza kuimba kocha atimuliwe na wengine baada ya mechi walimrushia chupa na makopo ya maji. Kwenye mchezo wa marudiano Yanga wakafungwa 3-0 na maamuzi ya kufutwa kazi kwa Zahera yakachukuwa nafasi.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya