US Open: Federer Atupwa Nje, Serena William Akitumia Dakika 44 Kutinga Robo Fainali

4th September 2019

WASHINGTON, Marekani -Bingwa mara tano wa michuano ya US Open kwa upande wa wanaume, Roger Federer ametupwa nje ya michuano hiyo baada ya kupokea kichapo cha kushtukiza kutoka kwa Mbulgaria, Grigor Dimitrov. Federer, 38, amemfunga Dimitrov katika michezo yote saba iliyopita lakini Mbulgaria huyo alipambana na kushinda kwa seti 3-6 6-4 3-6 6-4 6-2. Katika mchezo huo Federer alilazimika kupata tiba baada ya kuhisi maumivu ya mgongo hata hivyo aliendelea na kumaliza mchezo huo. Kwa ushindi huo sasa Dimitrov anayeshika nafasi ya 78 kwa ubora duniani atakutana na Mrusi, Daniil Medvedev kwenye mchuano wa robo fainali. Kipigo cha Federer katika hatua hii kimekuja siku mbili baada ya mbabe mwingine Novak Djokovic kuondoshwa baada ya kuhisi majeraha ya bega na kuamua kukubali kushindwa katikati ya mchezo. 44 tu kwa Serena Kwa upande wa kina dada, Serena Williams ametumia dakika 44 kumsambaratisha Mchina, Wang Qiang na kutinga robo fainali ya michuano ya US Open kibabe. Williams, 37, ameshinda kwa seti 6-1 6-0 kwenye mchezo wa upande mmoja ambao kama kawaida ulipigwa kwenye uwanja wa Arthur Ashe. Kwa matokeo hayo Williams ambaye ni mchezaji namba nane kwa ubora akiwa na mataji 24 ya grand slam atavaana na mchezaji namba tano kwa ubora Elina Svitolina raia wa Ukraine ambaye naye amemuondosha Johanna Konta katika mchezo mwingine wa mapema. "Nikiwa nacheza na mpinzani anayecheza vizuri basi huwa sina budi kucheza vizuri zaidi au kurudi nyumbani, na sipo tayari kurudi nyumbani kwa sasa," amesema Williams baada ya mchezo. Williams anafukuzia taji la kwanza la Grand Slam ambalo hakushinda tangu alipotoka kujifungua 2017. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya