Tennis: Ni Rafael Nadal Vs Daniil Medvedev Fainali Ya US Open

7th September 2019

NEW YORK, Marekani -Mcheza tenesi namba mbili kwa ubora kwa upande wa wanaume Rafael amefuzu kucheza fainali ya michuano ya US Open ambapo atacheza dhidi ya Mrusi, Daniil Medvedev siku ya Jumapili. Nadal, 33, amemfunga Matteo Berrettini kwenye mchezo wa nusu fainali kwa jumla ya seti 7-6 (8-6) 6-4 6-1 wakati Medvedev akimuondosha Grigor Dimitrov kwa ushindi wa seti 7-6 (7-5) 6-4 6-3 kwenye mchezo mwingine wa nusu fainali. Kwa matokeo hayo Nadal anapewa nafasi ya kushinda taji la 19 la Grand Slam ikiwa ni moja pungufu ya Roger Federer ambaye anashikilia rekodi ya kuwa na Grand Slam 20. Utabiri umetimia Medvedev alitabiriwa kuleta upinzani mkubwa dhidi ya Novack Djokovic, Nadal na Federer kwenye michuano hii na utabiri huo umetimia kwani amefanikiwa kutinga fainali na moja kati ya watu hao. Hata hivyo ni jambo la kusubiri kuona atasimama vipi dhidi ya Nadal ambaye yupo moto kuliko kawaida akiwa amepoteza alama mbili tu hadi kufika fainali. Kwa upande wa wanawake, fainali itakuwa ni kati ya Serena Williams ambaye atavaana uso kwa uso dhidi ya Bianca Andreescu. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya