Tennis:Andreescu Ambwaga Serena Williams Na Kushinda US Open, Avunja Rekodi Ya Sharapova

8th September 2019

CALIFORNIA, Marekani -Mwanadada Bianca Andreescu ameshangaza wengi ulimwenguni baada ya kufanikiwa kutwa taji la US Open kwa kumfunga mkongwe Serena Williams kwenye mchezo wa fainali uliopigwa alfajiri ya leo. Hili ni taji la kwanza la Grand Slam kwa Andreescu ambaye anatajwa kama mchezaji namba 15 kwa ubora duniani kwa upande wa wanawake. Williams, 37, hakuweza kuendana na kasi ya Mcanada huyo ambaye ameshinda kwa jumla ya seti 6-3 75. "Mwaka huu umekuwa ni wa ndoto zangu kuwa kweli," amesema Andreescu mwenye umri wa miaka 19 akiwaambia mashabiki. "Imekuwa ni zaidi ya kubarikiwa, nimefanya kazi kwa bidii sana hadi kufikia hatua hii ya kucheza kwenye hatua hii dhidi ya Serena ambaye ni mkongwe wa kweli kwenye huu mchezo," amesema Andreescu. Kwa upande wa Serena ambaye anakuwa amepoteza fainali ya nne mfululizo huku akiwa hajashinda Grand Slam tangu alipotoka kujifungua mwaka 2017 amesema kuwa Andreescu amecheza mechi nzuri na hivyo ni haki yake kushinda. "Amecheza kwa kiwango kikubwa mno, ninafurahi ameshinda, ilikuwa ni mechi nzuri sana ya fainali," amesema Williams. Andreescu anakuwa mcheza tenesi mdogo kushinda Grand Slam tangu Maria Sharapova alivyofanya hivyo mwaka 2006. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya