Ndondi: Hassan Mwakinyo Kupanda Ulingoni Oktoba 26

5th September 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania -Bondia nambari moja kwa uzito wa kati nchini, Hassan Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni Oktoba 26, mwaka huu kucheza pambano la kimataifa. Hata hivyo bado jina la mpinzani wake halijawekwa wazi na huku pia haijajulikana kama litakuwa ni pambano la ubingwa ama la kirafiki. Promota Juma Msangi amesema kuwa hadi sasa zaidi ya mabondia watano kutoka mataifa ya Marekani, Italia, Urusi, Ufilipino na Argentina wameonesha nia ya kutaka kupambana na Mwakinyo hivyo ni jambo la muda tu kabla ya pambano hilo kutangazwa rasmi. Akizungumza jijini Dar es salaam, Msangi amesema kuwa wiki ijayo ndio wanatarajia kuliweka hadharani jina la mpinzani wa Mwakinyo baada ya kuyapitia na kujua ubora wa kila bondia. "Tumepokea majina kutoka kwa wapinzani wa mataifa mbalimbali, bado hatujakaa kuchuja uwezo wa kila mmoja na kuangalia nani anatufaa, baada ya siku chache mbele tutakuwa na taaarifa kamili kuhusu pambano hilo," amesema Msangi. Kwa upande wake Mwakinyo ambaye ni balozi wa SportPesa, amesema kuwa amefanya maandalizi mazuri kwa muda mrefu na hivyo yupo tayari kwa pambano la aina yoyote bila kujali aina ya mpinzani. "Kwa upande wa maandalizi mimi sina shida, nimefanya mazoezi mengi ya maana na hivyo nipo tayari kwa ajili ya kupambana na yoyote kwa mchezo wa aina yoyote," amesema Mwakinyo. Imeandaliwa na Rahim Mohamed