Ndondi: Hassan Mwakinyo Aahidi Kutoa Dozi Nene Kwa Mfilipino

24th November 2019

DAR ES SALAAM,Tanzania- Baada ya tambo za kipindi kirefu hatimaye mabondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo na Mfilipino, Arnel Tinampay wamekutana leo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kulizingumzia pambano lao la Novemba 29.

Hassan Mwakinyo
Hassan Mwakinyo
SUMMARY

"Jamaa amepita njia ambayo siyo nzuri, kujileta kwangu ni sawa na kujitafutia maafa. Nitampiga hadi achakae kabisa," amesema Mwakinyo.

Mabondia hao wa uzito wa kati kila mmoja ametamba kumfanyia kitu mbaya mwenzie siku ya pambano huku tukio la kukutanishwa kwao leo likijawa na vibweka vya kila aina.

Tinampay ambaye anaelezwa kuwa anatoka kwenye kambi ya bondia bingwa wa dunia, Manny Pacquiao aliwasili nchini tangu Jumatatu iliyopita na amekuwa akiendelea na mazoezi yake hapa jijini Dar es salaam kama ilivyo kwa Mwakinyo.

Pambano hilo kwa mara ya kwanza litafanyika ndani ya uwanja wa Uhuru, Dar es salaam ambapo linatarajiwa kuvuta hisia za mashabikiwa wengi wa mchezo wa ngumi nchini.

Nitampiga Hadi Achakae

Mbele ya watu na waandishi wa habari waliojitokeza leo, Mwakinyo ambaye ni balozi wa kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa amesema kuwa anatarajia kutoa kipigo kizito kwa mpinzani wake huyo ambaye anajivunia rekodi yake bora nchini kwao.

"Jamaa amepita njia ambayo siyo nzuri, kujileta kwangu ni sawa na kujitafutia maafa. Nitampiga hadi achakae kabisa," amesema Mwakinyo.

Sina Wasiwasi

Naye Tinampay amesema kuwa licha ya kuwa atakuwa ugenini lakini bado hana wasiwasi dhidi ya mpinzani wake na anatarajia kumaliza mchezo kwa KO.

"Najua nipo ugenini lakini sina shaka kwa hilo, natarajia kumpiga na kumaliza mchezo kwa KO na kisha baada ya hapo atakuwa rafiki yangu," amesema Tinampay.

Maandalizi Tayari

Promota wa pambano hilo J Msangi amesema kuwa tayari kila kitu kimekaa sawa kuelekea pambano hilo na hivyo amewaita Watanzania wote waishio Dar es salaam pamoja na mikoa ya karibu kuja kushuhudia burudani ya masumbwi.

Imeandaliwa na Raheem Mohamed