NBA: Mambo 5 Tuliyojifunza Kwenye Wiki Ya Pili Ya Ligi Ya Kikapu Marekani

8th November 2019

TORONTO, Marekani- Ligi ya mpira wa kikapu ya Marekani NBA, imeingia kwenye wiki yake ya tatu na michezo inaendelea kupamba moto kweli kweli.

NBA
NBA
SUMMARY

Wakati majina mengine kama vile LeBron James, Kawhi Leonard, Giannis yakizidi kutamba kunako NBA ya msimu huu huko Houston Rockets yupo mwamba anaitwa James Harden ambaye naweza kusema kama anafukuza mwizi kimya kimya.

Hata hivyo kama ilivyokuwa kwenye wiki ya kwanza, wiki ya pili pia ilikuwa na mambo yake yakusisimua ambayo SportPesa News inakuletea japo kwa ufupi.

GSW Imeshikwa Pabaya

Kama kuna timu imeshikwa pabaya msimu huu basi moja wapo ni Golden State Warriors. Baada ya kutawala ligi hiyo kwa takribani misimu mitano iliyopita msimu huu GSW wamejikuta katika hali ngumu sana.

Tayari wamepoteza michezo sita kati ya nane waliyoshuka dimbani msimu huu hadi kufikia hivi sasa. Tatizo kubwa linalowakabili ni kuandamwa na majeruhi ambapo Stephen Curry na Klay Thompson wote ni majeruhi wa muda mrefu huku Draymond Green naye akipata majeruhi yatakayomfanya akose mechi kadhaa.

Kombo Ya Lebron & Davis Hatari

Tangu walipofungwa kwenye mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya majirani zao LA Clippers, timu ya LA Lakers imeibuka na ushindi kwenye michezo yao yote sita iliyofuatia.

Mafanikio hayo hayakuja hivi hivi bali ni kutokana na ushirikiano mzuri kati ya LeBron James na Anthony Davis ambao wamekuwa mwiba kwa timu pinzani kwenye kila mchezo.

Kawhi Leonard Usajili Bora Clippers

Kabla ya kuanza kwa msimu timu zilipata nafasi ya kusajili na kila mmoja alifanya hivyo. Hata hivyo niseme tu Kawhi Leonard aliyesajiliwa na LA Clippers akitokea Toronto Raptors unaweza ukawa ndiyo usajili bora hadi hivi sasa.

Mchezaji huyo ambaye alifanya kazi kubwa kuhakikisha anaipatia Raptors taji lao la kwanza la NBA ameendeleza moto wake ndani ya timu ya Clippers na kuifanya kuwa na makali ambayo hawakuwahi kuwa nayo hapo awali.

James Harden Anafukuza Mwizi Kimya Kimya

Wakati majina mengine kama vile LeBron James, Kawhi Leonard, Giannis yakizidi kutamba kunako NBA ya msimu huu huko Houston Rockets yupo mwamba anaitwa James Harden ambaye naweza kusema kama anafukuza mwizi kimya kimya.

Anafanya mabalaa ambayo hayapati sana kiki pengine ni kutokana na aina ya timu anayocheza lakini amekuwa ni nguzo muhimu kupita maelezo.

Kwenye mechi 8 walzoshuka uwanjani msimu huu timu yake imeshinda mara 5 huku ikipoteza michezo mitatu lakini Harden amekuwa aking'aa kwenye kila aina ya takwimu baada ya kuisha kwa mchezo.

Kevin Durant Maji Ya Shingo

Baada ya kutamba kwa miaka mitatu akiwa na Golden State Warriors, Kevin Durant aliona ni vyema aondoke akaanze maisha yake mapya kwenye timu nyingine ambapo alijiunga na Brookly Nets mwanzo wa msimu huu.

Hata hivyo mambo siyo mazuri huko alipokwenda kama ilivyo kwenye timu aliyotoka. Hadi hivi sasa Brooklyn Nets wamecheza mechi saba na wameshinda mechi tatu tu huku yeye mwenyewe takwimu zake zikiwa siyo nzuri hata kidogo.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya