Maoni: Jinamizi la Mbwana Samatta Na Simon Msuva Kuendelea Kuitafuta Stars Huko Sudan?

17th October 2019

KHARTOUM, Sudan- Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars siku ya Ijumaa itakuwa ni kibarua kizito mbele ya Sudan pale timu hizo zitakapoumana kugombea nafasi ya kushiriki michuano ya CHAN.

Mbwana Samatta
Mbwana Samatta
SUMMARY

Ningependa kuona mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kwenye mchezo wa kesho kwani ushindi kwa Stars si tu utailetea heshima nchi bali itakuwa pia ni fursa kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani kwenda kujiuza CHAN.

Kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es saalam, Tanzania timu ya Sudan ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuweza kusonga mbele.

Hii si mara ya kwanza kwa timu za Stars na Sudan kukutana kwenye hatua kama hiyo ya kuwania kufuzu CHAN. Mwaka 2011 mimamba hao walikutana na Stars wakiwa chini ya kocha Marcio Maximo walifanikiwa kuibuka na jumla ya ushindi wa 5-2 baada ya michezo miwili.

Safari hii mambo yanaonekana kuwa magumu kidogo kwa Stars ambao sasa watahitajika kufunga mabao zaidi ya mawili kama watahitaji kutinga kwenye michuano ya CHAN itakayofanyika Cameroon.

Swali ambalo wengi wanajiuliza ni je namna gani timu hiyo itaweza kufunga mabao hayo zaidi ya mawili ilhali tangu kocha Etiene Ndayiragije akaimu nafai ya kocha Mkuu wa Stars timu hiyo imekuwa na uhaba wa mabao?

Tayari Ndayiragije ameshaiongoza Stars kwenye mechi 6. Kwenye michezo hiyo wameambulia sare tano ndani ya dakika 90 za mchezo (mechi mbili wakashinda kwa penati) na mechi moja wamefungwa ambayo ndiyo hiyo dhidi ya Sudan.

Kwenye mechi hizo 6 ambazo zimetangulia mabao ambayo yamefungwa ni mawili tu na yote yamefungwa na wachezaji ambao wanacheza nje ya nchi (Simon Msuva, Mbwana Samatta0 kwa lugha nyepesi naweza kusema kuwa yamefungwa na wachezaji ambao hawahusiki na mchezo wa kesho.

Mara ya mwisho kwa Stars kufunga walau mabao mawili kwenye mchezo mmoja ilikuwa ni mwezi wa Julai wakati wa mashindano ya Afcon ambapo walipokea kichapo cha 3-2 kutoka kwa Kenye na kama kawaida mabao ya Stars yalifungwa na Msuva na Samatta.

Kulingana na takwimu zilivyo kwa hivi sasa inaonesha wazi kuwa Samatta na Msuva ndiyo washambuliaji bora wa Stars na kwa bahati mbaya hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza na Sudan kwani wachezaji wanaohusika ni wale wanaocheza ligi ya ndani tu.

Kwenye kipindi kama hiki nilitegemea kuona washambuliaji wengine wanaocheza ligi ya ndani wakiitumia nafasi hii vizuri nakuonesha makucha yao. 

Wachezaji wazawa wanaocheza ligi ya ndani kama vile Shabin Chilunda, Ayoub Lyanga na wengine hii ilikuwa ni fursa yao muhimu ya kuanza kutengeneza ufalme wao ndani ya Stars.

Hata waliobuni mashindano hayo walitegemea kutoa fursa kwa wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kwenda kucheza nje ya nchi ili waonekane kimataifa.

Sina shaka na wachezaji wanaocheza kwenye idara ya ulinzi, kiungo hata sehemu ya golini kwa makipa. Kiukweli wanafanya kazi nzuri.

Lakini wachezaji wetu hasa wanaocheza upande wa ushambuliaji wanashindwa kuitumia fursa hii muhimu kwao na kuonesha kuwa Stars bila Msuva na Samatta haiendi.

Kwenye mchezo dhidi ya Sudan uliofanyika hapa Dar es salaam, Stars walitengeneza nafasi nyingi nzuri za kufunga lakini washambuliaji walishindwa kuzitumia.

Ningependa kuona mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kwenye mchezo wa kesho kwani ushindi kwa Stars si tu utailetea heshima nchi bali itakuwa pia ni fursa kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani kwenda kujiuza CHAN.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya