Mambo Makubwa Tuliyoshuhudia Tangu Kuanza Msimu Wa Ligi Kuu Bara

5th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Ligi Kuu Tanzania Bara kama zilivyo ligi nyingi duniani ilianza mwishoni wa mwezi Agosti, mwaka huu.

Yanga SC
Yanga SC
SUMMARY

Kijana huyo alisajiliwa akitoka Allience ya Mwanza na usajili wake haukuwa na makeke mengi kama wachezaji wengi lakini kwenye mechi nne tu alizocheza tayari ameonesha kuwa yeye ni mchezaji wa aina gani na ambaye mashabiki wa Yanga itabidi wamuangalie zaidi kwenye mechi 34 walizobakiwa nazo.

Hadi kufikia sasa tayari tumeshuhudia matukio kadhaa ya kusisimua wakati timu zikiwa zinayoyoma kumaliza mechi zao za msimu huu.

Tangu kuanza kwake kumekuwa na mambo mengi ambayo yamekuwa yakijiri ndani na nje ya uwanja lakini kwa kifupi sana haya ni yale ambayo naamini yatakuwa ni yenye mvuto zaidi.

Panga Pangua Ya Ratiba

Kama ilivyokuwa kwenye misimu mingine iliyopiota, msimu huu pia suala la ratiba limeendelea kuumiza vichwa vya wadau wa soka.

Mara nyingi suala hili la upangaji na upanguaji wa ratiba limekuwa likisababishwa na kambi za timu ya taifa pamoja na timu ambazo huwa zinashiriki michuano ya kimataifa.

Hapa ninapoongea na wewe ligi hiyo haieleweki ipo mzunguko wa ngapi kwani zipo tikmu ambazo zimeshaceheza hadi mechi 10 lakini pia zipo timu ambazo zimecheza mechi nne tu.

Kwa kifupi ni kwamba suala hili limeshakuwa sugu na ni wakati sasa wadau kulikubali ili liwe kama moja kati ya vitu vya kuvutia ndani ya ligi yetu.

Umwamba wa Meddie Kagere

Meddie Kagere ana mabao saba msimu huu na ndiye kinara kwenye ufungaji Tanzania Bara.

Msimu uliopita mchezaji huyo pia alishinda tuzo ya ufungaji bora. Hii maana yake ni kwamba Kagere amekuwa mwamba wa ligi kuu kwa misimu hii miwili.

Mtibwa Sugar Waanza Kivingine

Kwa misimu takribani minne kama siyo mitatu, Mtibwa Sugar wamekuwa wakianza ligi kwa nguvu kubwa kupita maelezo.

Wamekuwa wakizoa alama kwenye mechi za awali kwa viwanja vya nyumbani na ugenini. Hata hivyo mambo yamekwenda tofauti msimu huu wakianza ligi kwa kusuasua kuliko ilivyokuwa kawaida.

Pengine hili limechangiwa na kubadilisha uwanja ambapo TFF, wamewaamuru kuacha kuutumia uwanja wao wa Manungu hadi utakaporekebishwa na kukidhi viwango, hivyo kwasasa wanalitumia dimba la Jumhuri kwenye mechi zao za nyumbani.

Simba Kutetea taji?

Timu ya Simba ambao ni mabingwa mara mbili mfululizo wameanza ligi ya msimu huu kwa kishindo wakishinda kwenye mechi sita mfululizo kabla ya mbio zao kwenda kuishia kwa Mwadui.

Hata hivyo baada ya kipigo kutoka kwa Mwadui, timu hiyo imeweza kuinuka na kushinda 4-0 dhidi ya Mbeya City kwenye mechi iliyopita.

Uwezo walioonesha Simba tangu msimu ulipoanza ni wa hali ya juu na ni vigumu kuona jinsi gani watazuiwa wasichuku tena ubingwa msimu huu.

Singida United Inapumulia Mashine

Hadi kufikia sasa Singida United wamecheza mechi 10 za ligi kuu lakini huwezi kuamini hawajawahi kuambulia ushindi hata siku moja.

Timu hiyo inaburuza mkia wakiwa na alama nne tu walizokusanya kwa kutoa sare ikiwemo kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya Jumamosi.

Hadi sasa wameshakuwa chini ya makocha wawili, wakianza msimu na Fred Minziro na sasa wapo na Ramadhani Nswanzerimo lakini mambo bado kabisa. 

Kama unakumbuka vizuri timu hiyo ilikuja ligi kuu misimu miwili iliyopita na ilileta changamoto kubwa kiasi watu kuitabiria mambo mazuri mbeleni lakini hadi sasa hali si hali na wanalichungulia tundu la kutokea.

Balama Mapinduzi Usajili Bora Yanga

Unaweza ukasema kuwa Yanga ndiyo waliosajili wachezaji wengi kuliko timu yoyote kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu Bara.

Wamesaji wachezaji wakimataifa ambao wengine walikuja kwa mbwembwe za kufa mtu. Hata hivyo huwezi kupingana na ukweli kuwa kwenye usajili wao wote waliofanya wa wachezaji takribani 14, Balama Mapinuzi ndiyo mchezaji nyota hadi hivi sasa.

Kijana huyo alisajiliwa akitoka Allience ya Mwanza na usajili wake haukuwa na makeke mengi kama wachezaji wengi lakini kwenye mechi nne tu alizocheza tayari ameonesha kuwa yeye ni mchezaji wa aina gani na ambaye mashabiki wa Yanga itabidi wamuangalie zaidi kwenye mechi 34 walizobakiwa nazo.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya