Ligi Kuu Bara: Yanga Ya Boniface Mkwasa Kuanza Kazi Mbele Ya Ndanda Leo?

8th November 2019

MTWARA, Tanzania- Ligi Kuu bara inaendelea tena leo kwa michezo mitatu kupigwa kwenye viwanja tofauti. ambapo macho na masikio yatakuwa huko mkoani Mtwara wenyeji Ndanda FC wakiwaalika Yanga.

Yanga SC
Yanga SC
SUMMARY

Yanga ndiyo timu iliyocheza michezo kidogo zaidi ukilinganisha na wengine, wameshuka dimbani mara nne wakiibuka na ushindi mara mbili, sare moja na wamepoteza mchezo mmoja hivyo wana alama 7 ambazo ni sawa na za Ndanda ambao wameshuka dimbani mara 8 msimu huu.

Naweza kusema hii ndiyo mechi kubwa kwa siku ya leo hasa ukizingatia ukubwa wa Yanga na aina ya mchezo watakaokutana nao leo.

Yanga wanaingia kwenye mchezo wa kwanza bila ya aliyekuwa kocha wao mkuu Mwinyi Zahera ambaye alifungashiwa virago mwanzo wa wiki hii na nafasi hiyo sasa inakaimiwa na Charles Boniface Mkwasa akisaidiwa na Said Maulid.

Mchezo huu ni watano kwa Yanga msimu huu baada ya kuwa bize na ratiba za mechi za kimataifa tangu mwanzo wa msimu.

Yanga wamekuwa na wakati mgumu sana mara nyingi wanapocheza na Ndanda FC kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Kwenye misimu mitano iliyopita tangu Ndanda waliurudi kucheza ligi kuu Yanga wameshinda mara moja tu ndani ya uwanja huo ikiwa ni msimu wa 2017-18 ambapo waliibuka na ushindi wa 2-1.

Rekodi inaonesha kuwa huu utakuwa ni mchezo wa 11, kwenye michezo 10 iliyopita Yanga wameshinda mara 4, sare 5 na Ndanda wameshinda mara 1.

Mechi zote mbili za msimu uliopita zilikwisha kwa sare ya 1-1. Kwa takwimu hizo ni wazi kabisa zinaonesha ugumu wa mchezo wa leo hasa kwa Yanga ambao wanaingia bila ya wachezaji 8 ambao wanakosekana kwasababu mbalimbali.

Ally Ally, Paul Godfrey, Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Lamine Moro, Cleofas Sospters, Juma Balinya, Maybin Kalengo hawa ni wachezaji wa Yanga ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha leo kwa majibu wa taarifa iliyotolewa na meneja wa kikosi hicho, Dismas Teni.

Yanga ndiyo timu iliyocheza michezo kidogo zaidi ukilinganisha na wengine, wameshuka dimbani mara nne wakiibuka na ushindi mara mbili, sare moja na wamepoteza mchezo mmoja hivyo wana alama 7 ambazo ni sawa na za Ndanda ambao wameshuka dimbani mara 8 msimu huu.

Mechi nyingine za leo

KMC v Kagera Sugar

Azam v Biashara United

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya