Ligi Kuu Bara: Mbao FC vs Yanga Hatumwi Mtoto Dukani CCM Kirumba Leo
22nd October 2019
MWANZA, Tanzania- Kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo jioni kutakuwa na mechi ya kukata na mundu mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara ambao utawakutanisha wenyeji Mbao FC watakao wakaribisha Yanga ya Dar es salaam.

Kwa ujumla kabla ya mchezo wa leo, timu hizo zimekutana mara saba kwenye michuano yote na Yanga ameshinda mara nne huku Mbao wakishinda mara tatu zote ikiwa ni CCM Kirumba.
Mchezo huo ni wakupaniana kwa pande zote mbili na kama unakumbuka Yanga wamekuwa wakipata tabu sana kucheza dhidi ya Mbao pindi timu hizo zinapokutana kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Huu utakuwa ni mchezo wa saba kwa wenyeji Mbao ambao tayari wameshashuka dimbani mara sita na kujikusanyia alama 7 huku wapinzani wao Yanga wakiwa na alama nne baada ya kushuka dimbani mara tatu.
Mchezo wa leo unaweza kuhesabika pia kama maandalizi ya mwisho kwa Yanga ambao siku ya Jumapili kwenye uwanja huo watakuwa na kibarua cha kuwakaribisha Pyradids ya Misri kwenye mchezo wa mtoano wa kombe la Shirikisho Afrika.
Hali ya vikosi
Kwa upande wa Mbao wanatarajia kuwa na kikosi chao kamili ambacho kimecheza mechi mbalimbali za ligi kuu msimu huu.
Yanga wao bado wanasumbuliwa na baadhi ya wachezaji majeruhi ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo huu.
Mlinzi wa pembeni Paul Godfrey "Boxer" amerejea mazoezini lakini bado anaonekana kutokuwa fiti kwa ajili ya mchezo huu hivyo hivyo kwa mshambuliaji Issa Bigirimana.
Wachezaji wengine ambao walikosa mchezo uliopita dhidi ya Coastal Unioni kama vile nahodha Pappy Tshishimbi, Patrick Sibomana na Lamine Moro leo wanaweza wakawa tayari kwa mchezo.
Hata Kelvin Yondani ambaye aliumia kwenye mchezo wa Coastal Union na kufanya hadi kukosa michezo ya timu ya taifa amerejea mazoezini na leo huenda akawa ni sehemu ya kikosi.
Historia Ya Timu Zinapokutana
Tangu Mbao FC walivyopanda daraja kwenye msimu wa 2016-17 wamecheza dhidi ya Yanga mara sita kwenye michezo ya ligi kuu na mara moja kwenye mchezo wa kombe la FA.
Katika hizo mara sita walizokutana kwenye michezo ya ligi kuu, mechi tatu zimefanyika uwanja wa taifa, Dar es salaam Yanga wameshinda mechi zote bila Mbao kupata bao hata moja.
Kwenye mechi tatu zilizofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mbao wameshinda mara mbili na wamekubali kipigo mara moja kwenye mchezo wao wa msimu uliopita.
Hata hivyo mbali na ligi kuu timu hizo pia ziliwahi kukutana kwenye mchezo wa kombe la FA ambapo mechi ilichezwa CCM Kirumba na Yanga walila kwa mabao 2-0.
Kwa ujumla kabla ya mchezo wa leo, timu hizo zimekutana mara saba kwenye michuano yote na Yanga ameshinda mara nne huku Mbao wakishinda mara tatu zote ikiwa ni CCM Kirumba.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya