Ligi Kuu Bara: Makame Na Molinga Safi, Kipi Kimejiri Yanga v Coastal Union?

7th October 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania -Yanga wamepata ushindi wao wa kwanza msimu huu ndani ya ligi kuu bara wakiwafunga Wagosi Wakaya, Coastal Union kwa bao 1-0.

Yanga vs Coastal Union
Yanga vs Coastal Union
SUMMARY

Wapenzi na mashabiki wa Yanga wamekuwa hawaridhishwi na namna timu yao inavyocheza na wengine wamefika mbali kwa kusema kuwa usajili uliofanywa ni mbovu hasa kwa wachezaji wa kimataifa na wengi wao hawafikii uwezo wa wachezaji wa ndani.

Bao la Yanga kwenye mchezo huo limefungwa na kiungo Abdulaziz Makame kwenye dakika ya 51 kipndi cha pili na kufanya Wanajangwani hao kufikisha alama nne baada ya kushuka dimbani mara tatu msimu huu.

Mbali na matokeo lakini dawati la SportPesa News lina mambo mengine ambayo limeyanasa kwenye mchezo huo uliokuwa mkali na wa kuvutia.

Mwamuzi Ameshindwa Kumudu Mchezo

Mwamuzi aliyechezesha mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union, Abuubakar Mturo kutoka Lindi ameshindwa kumudu kusimamisha sheria 17 za soka na alionekana akiyumba kwenye baadhi ya matukio huku akikosa mawasiliano mazuri na wasaidizi wake.

Mfano kuna rafu ambazo wamechezewa wachezaji wa Yanga kama vile Deus Kaseke na Kelvin Yondani hadi kupelekea kuumia na kufanyiwa mabadiliko zote hakuziona.

Hata kwa upande wa bao walilofunga Yanga ingawa yeye ndiye aliyekuwa mwenye maamuzi ya mwisho lakini hakuwasiliana vyema na wasaidizi wake kitu ambacho kimeacha gumzo kuhusu goli hilo.

Makame Anawaziba Midomo

Takribani wiki moja sasa imepita tangu kiungo mpya wa Yanga Abdulaziz Makame aingie kwenye vinywa vya mashabiki wa mpira wa Tanzania. Hii ni baada ya kujifunga bao ambalo limewaondosha Yanga kwenye ligi ya mabingwa wakati wanacheza na Zesco, Zambia.

Hata hivyo kejeli na maneno yote hayo hayajamkatisha jamaa tamaa na tangu arejee Tanzania ameshacheza mechi mbili za ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union na bado ameonesha kuwa yeye ni mchezaji wa aina gani.

Anautulivu mkubwa akiwa na mpira lakini pia anakaba kwa nidhamu na pia anajua kusoma sehemu zenye hatari na kufika kwa wakati kutatua shida.

Molinga Mambo Safi

Baada ya kuanza kwa kususua sana kufikia hatua ambayo washabiki wake wakaanza kumkataa. hatimaye mshambuliaji mwenye miraba minne David Molinga "Falcao" ameanza kuonesha uwezo wake mkubwa uwanjani.

Kwenye mechi dhidi ya Coastal Union hakufanikiwa kufunga bao lakini alikuwa ni mchezaji hatari zaidi kwa upande wa Yanga wakati wakiwa wanakwenda kushambulia.

Kama si umakini wa mabeki wa Coastal Union jamaa jana angefunga tena ikiwa ni siku chache baada ya kuinusuru Yanga na kichapo kutoka kwa Polisi Tanzania.

Noel Mwandila Uwezo Wake Siyo Mkubwa

Ni kweli Noel Mwandila ni kocha msaidizi tu lakini nadhani kazi ya usaidizi moja wapo ni hii ya kushika timu pindi kocha mkuu anapokuwa hayupo. 

Hata hivyo rekodi ya Mwandila pindi anapokuwa ameachiwa kuongoza timu inakuwa si ya kuvutia tangu kipindi kile wakati George Lwandamina yupo.

Kwenye mechi mbili ambazo Yanga wamecheza bila ya kocha wake mkuu Mwinyi Zahera ambaye anatumikia adhabu ya mechi tatu timu imekuwa ikicheza bila maelewano mazuri.

Ni muda muafaka sasa kwa Yanga kutathimini na kufanya maamuzi ya aidha kuajiri kocha mwingine msaidizi ambaye ataweza kumsaidia Zahera kwa ufasaha.

Mwinyi Zahera Amekubali Yaishe?

Wapenzi na mashabiki wa Yanga wamekuwa hawaridhishwi na namna timu yao inavyocheza na wengine wamefika mbali kwa kusema kuwa usajili uliofanywa ni mbovu hasa kwa wachezaji wa kimataifa na wengi wao hawafikii uwezo wa wachezaji wa ndani.

Kwenye mchezo wa jana kocha Mwinyi Zahera aliamua kupunguza idadi kubwa ya wachezaji wa kimataifa kwenye kikosi chake na kuwapa wachezaji wazawa ambao nao bila ajizi hawakuamuangusha.

Wachezaji pekee wakimataifa waliocheza jana ni David Molinga na Farouk Shikalo huku Mustapha Seleman akipata nafasi ya kuingia kipindi cha pili mwishoni baada ya Kelvin Yondani kuumia.

Sasa swali linabaki ni je, Zahera amekubali yaishe na kuanza kuwapa nafasi wazawa tu?

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya