Lallana Ainusuru Liverpool Kupokea Kipigo Cha Kwanza EPL Mbele Ya Manchester United

20th October 2019

MANCHESTER, Uingereza- Klabu ya Manchester United imefanikiwa kuwasimamisha Liverpool kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuwalazimisha sare ya 1-1 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Uingereza uliofanyika kwenye uwanja wa Old Trafford.

Adam Lallana
Adam Lallana
SUMMARY

Mabadiliko aliyofanya kocha Jurgen Klopp ya kumtoa nahodha Jordan Henderson na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Lallana yalizaa matunda kwani zikiwa zimesalia dakika 6 kabla ya mpira kumalizika Liverpool walichomoa bao kupitia mchezaji huyo raia wa Uingereza.

Mechi hiyo ilikyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi duniani imechezwa kwa mtindo wa kuviziana kila kocha akijaribu kutumia mashambulizi ya kushtukiza kwa ajili ya kupata mabao.

Manchester United ndiyo walionufaika na mfumo huo kwenye dakika ya 32 kipindi cha kwanza baada ya kufanya shambulizi la kasi lililowajumuisha kiungo McTominay aliyepipa mpira kwa winga Daniel James pembeni na yeye bila kuchelewa alimimini majaro ndani yaliyomaliziwa vizuri na Marcus Rashford.

Kwenye sekunde za mwisho kabla ya timu kwenda mapumziko Liverpool nao walifanya shambulizi la mpira mrefu uliomkuta Sadio Mane ambaye alipambana na mlinzi Victor Lindelof kabla ya kupachika bao kambani.

Hata hivyo bao hili lilikataliwa mara baada ya mwamuzi wa mchezo huo Martin Aktson kuthibitisha kupitia VAR kuwa Mane alikuwa ameshika wakati akijaribu kuuweka mpira kwenye himaya yake.

Kipindi cha pili Liverpool walionekana kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa wakipiga pasi nyingi katikati na pembeni ya uwanja. Hata hivyo pasi hizo zilikuwa hazina madhara kwani ulinzi wa Man United chini ya Harry Maguire ulisimama imara kuondosha hatari zote.

Mabadiliko aliyofanya kocha Jurgen Klopp ya kumtoa nahodha Jordan Henderson na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Lallana yalizaa matunda kwani zikiwa zimesalia dakika 6 kabla ya mpira kumalizika Liverpool walichomoa bao kupitia mchezaji huyo raia wa Uingereza.

Kwa mataokeo hayo, Liverpool wanaendelea kubaki kileleni kwa tofauti ya alama sita dhidi ya Manchester City walio kwenye nafasi ya pili.

Nao Man United wanasogea hadi kwenye nafasi ya 13 wakiwa na alama zao 10 baada ya kushuka dimbani mara 9.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya