Kwaheri Ya Kuonana: Yanga Yampa Mkono Wa Kwaheri Mwinyi Zahera, Mkwasa Akikaimu Kwa Muda

5th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Hayawi Hayawi, Sasa Yamekuwa! Hatimae uongozi wa Yanga umetangaza rasmi kuachana na kocha wao mkuu Mwinyi Zahera ikiwa ni siku mbili tu tangu timu ilipotolewa kwenye michuano ya Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids.

Mwinyi Zahera
Mwinyi Zahera
SUMMARY

Zahera amefanikiwa kuwaongoza Yanga kwenye michezo 50 ambayo inajumlisha ligi kuu na michuano ya kimataifa tu.

Uongozi wa Yanga umetangaza maamuzi hayo leo muda mfupi huku Charles Mkwasa akitajwa kukaimu nafasi hiyo kwa muda kabla ya maamuzi ya kutamtangaza kocha mpya.

Yanga wamefikia maamuzi hayo ikiwa ni siku mbili tu tangu walipotolewa kwenye michuano ya kimataifa kwanza na Zesco United kwenye ligi ya mabingwa lakini pia na Pyramids kwenye kombe la Shirikisho ambapo walipokea kichapo cha jumla ya mabao 5-1 kwenye michezo miwili ya nyumbani na ugenini.

Kwenye ligi kuu hadi sasa Yanga wamecheza mechi 4 wakiwa wameshinda 2 wamefungwa moja na wamekwenda sare mchezo 1. Mchezo wao unaofuata wa ligi kuu ni dhidi ya Ndanda ambao umepangwa kufanyika Mtwara, Novemba 8.

Majina ambayo yanatajwa kurithi nafasi ya Zahera tangu awali ni Hans van Pluijum, Kim Poulsen huku jina la kocha wa Bandari ya Kenya, Ben Mwalala likionekana kushika kasi zaidi kwa kipindi cha hivi karibuni.

Wapi Alikosea Mwinyi Zahera?

Mwinyi Zahera siyo kocha mbaya kama wengi wanavyoweza kudhani na hata sababu zakufutwa kwake kazi sidhani kama zitaegemea sana kwenye kiwango cha timu.

Chini ya kocha Zahera timu ya Yanga ilikuwa haivutii sana kiuchezaji lakini ilikuwa ikipata matokeo ambayo wakati mwingine hata mashabiki walikuwa hawayategemei.

Kikosi cha Yangakwa misimu miwili iliyopita siyo kizuri ukilinganisha na watani zao Simba lakini Zahera alikuwa anapambana kwenye shida na raha kuhakisha walau anapata matokeo chanya.

Hata hivyo kawaida yake ya kutoa maneno hovyo tena hadharani akiwasema viongozi ama wachezaji nadhani inaweza kuwa ni moja kati ya sababu zilizomfanya kuondolewa kwenye nafasi yake.

Kuna maneno ambayo amekuwa akiongea kwenye vyombo vya habari ambapo mara nyingine huwa yana ukweli lakini amekuwa akitumia njia ambayo si sahihi kufikisha ujumbe wake.

Takwimu zake zipoje?

Zahera lilikuwa ni jina jipya kwenye vinywa vya mashabiki wa soka nchini na alikabidhiwa timu mwishoni wa msimu wa 2017-18 akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake George Lwandamina ambaye aliikimbia timu kutokana hali ya ukata wa klabu.

Hata hivyo Zahera baada ya kutajwa kuwa kocha wa timu hiyo hakuweza kuanza kazi mara moja kutokana na matatizo ya vibali vyake vya kufanyia kazi na ilimbidi asubiri kwa kipindi kirefu bila kukaa kwenye benchi.

Alianza kazi rasmi Agosti, 2018 wakati wa mchezo wa hatua ya makundi kombe la shirikisho ambapo aliiongoza Yanga kushinda 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria na huo ndiyo ulikua ushindi pekee kati ya mechi sita walizocheza kwenye hatua hiyo.

Alianza kibarua chake cha kwanza kwenye ligi kuu msimu uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar na walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Tangu hapo, Zahera amefanikiwa kuwaongoza Yanga kwenye michezo 50 ambayo inajumlisha ligi kuu na michuano ya kimataifa tu.

Kwenye michezo hiyo, Zahera alikuwa kocha wa Yanga kwenye michezo 42 ya ligi kuu (msimu uliopita na msimu huu) ambapo timu yake imepata ushindi mara 29 wakifungwa mara 7 na kutoka sare mara mbili.

Kwenye michezo ya kimataifa, Zahera ameiongoza Yanga kwenye mechi 8 ambapo wamepata ushindi mara mbili, wametoka sare mara mbili na wamepokea kichapo mara nne.

Jumla ya mabao ambayo Yanga wamefunga kwenye ligi kuu ni 57 na wamefungwa mabao 31, hiyo ni tangu msimu uliopita.

Kwenye michuano ya kimataifa, Yanga ndani ya mechi 8 Yanga wamefunga 7 na kufungwa mabao 11.

Mchezaji ambaye amefunga mabao mengi chini ya kocha Zahera ni Heritier Makambo ambaye alifunga jumla ya mabao 18 kwenye michuano yote.

Kwenye utawala wa Zahera timu ya Yanga imeongozwa na manahodha wa tatu tofauti akianza na Kelvin Yondani ambaye alichukuwa kijiti kutoka kwa Nadir Haroub msimu uliopita.

Hata hivyo Yondani hakumaliza msimu akiwa nahodha baada ya kuvuliwa na kuvalishwa Ibrahim Ajib ambaye naye baada ya kumalizika kwa msimu uliopita alitimkia Simba.

Nahodha wa Yanga msimu huu ni Papy Tshishimbi na amekuwa akiongoza kwenye mechi mbalimbali msimu huu akisaidiwa na Juma Abdul ambaye huwa anavaa ikitokea Tshishimbi hayupo uwanjani.

Katika misimu aliyokaa ndani ya Yanga ameshiriki michuano mbalimbali ikiwemo ligi kuu bara, kombe la FA, ligi ya mabingwa Afrika, kombe la shirikisho Afrika, kombe la mapinduzi na hajawahi kushinda taji lolote.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya