Kufuzu CHAN: Taifa Stars Yapindua Meza Kibabe Sudan Na Kutinga CHAN Cameroon 2020

19th October 2019

KHARTOUM, Sudan- Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefanikiwa kutinga kwenye michuano ya CHAN 2020 nchini Cameroon baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuwaondosha Sudan ambao walikuwa wananafasi kubwa ya kusonga mbele.

Taifa Stars
Taifa Stars
SUMMARY

Mshambuliaji Ditrim Nchimbi ambaye anacheza kwenye klabu ya Polisi Tanzania jina lake lilikuwa la mwisho kujumuishwa kikosini ndiye aliyeibuka shujaa baada ya kufunga bao la ushindi.

Mabao ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Erasto Nyoni aliyefunga kwa njia ya mpira wa adhabu na kisha Ditrim Nchimbi aliyemalizia kazi nzuri ya Shaban Chilunda yametosha kuwapa Stars ushindi huo muhimu wa ugenini.

Sudan waliingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na faida ya uongozi wa bao 1-0 kwa kutokana na ushindi walioupata nchini Tanzania takribani mwezi mmoja uliopita.

Hata hivyo ushindi walioupata Stars wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa leo umefanya matokeo kuwa 2-2 a hivyo Tanzania kusonga mbele kwa faida ya kufunga mabao mengi ugenini.

Huu unakuwa ni ushindi wa kwanza ndani ya dakika 90 kwa kocha Etiene Ndayiragije tangu akabidhiwe kikosi cha Stars akirithi mikoba ya Emmanuel Amunike.

Hapo awali kocha huyo aliiongoza Stars kwenye mechi sita wakienda sare mara tano na kufungwa mara moja huku katika sare hizo tano michezo miwili walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati.


Mara ya mwisho Stars kushiriki michuano ya CHAN ilikuwa ni mwaka 2009 chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mbrazil, Marcio Maximo.

Ushindi huu unakuwa ni neema kwa watanzania ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakishuhudia timu zao zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Michuano ya CHAN inahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani tu lakini kama haujasahau mapema mwezi Julai, mwaka huu kikosi cha Stars pia kilipata nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya Afcon ikiwa ni mara yao ya kwanza kwa kipindi cha miaka 39.

Ditrim Nchimbi Hajamuangusha Kocha Wake

Mshambuliaji Ditrim Nchimbi ambaye anacheza kwenye klabu ya Polisi Tanzania jina lake lilikuwa la mwisho kujumuishwa kikosini ndiye aliyeibuka shujaa baada ya kufunga bao la ushindi.

Nchimbi hakuitwa kwenye kikosi ambacho kilitangazwa awali lakini alikuja kuongezwa siku moja baada ya kufunga mabao matatu "Hat Trick" kwenye mchezo wa ligi kuu bara ambapo timu yake ilitoka sare ya 3-3 dhidi ya Yanga.

Kocha Etiene Ndayiragije unaweza kusema kuwa alichungulia vyema kuliongeza jina la mchezaji huyo kwani limemletea ushindi wake wa kwanza baada ya mechi sita tangu apewe timu kutoka kwa Emmanuel Amunike.

Erasto Nyoni Atimiza Ahadi

Kabla ya mchezo wa leo mlinzi wa kati wa timu hiyo anayecheza Simba, Erasto Nyoni aliahidi watanzania kuwa mchezo wa leo ni wa kufa au kupona na alisema kuwa watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.

Kauli hiyo imetimia baada ya timu kufanya vizuri kwa kuibuka na ushindi huku yeye pia akifunga bao muhimu la kusawazisha kwenye mchezo huo.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya