Kelvin Yondani Aongeza Orodha Ya Majeruhi Yanga

9th October 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Licha ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa na kocha Etiene Ndayiragije lakini inaelezwa kuwa mlinzi wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ni majeruhi.

Kelvin Yondani
Kelvin Yondani
SUMMARY

Wachezaji wengine ambao wapo nje kwa majeruhi ni Pappy Tshishimbi, Patrick Sibomana, Lamine Moro, Paul Godfrey, Mohamed Isaa, Rafael Daud, Sadney Urikhob.


Yondani aliumia kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union na alishindwa kumaliza mchezo wakati Yanga wanaibuka na ushindi wa 1-0.

Kabla ya hapo tayari kocha Ndayiragije alikuwa ameshamjumuisha kwenye kikosi chake ambacho mwezi huu kitakuwa na michezo miwili dhidi ya Rwanda, Oktoba 14 (Kirafiki) na dhidi ya Sudan, Oktoba 18 (CHAN).

Akizungumza na SportPesa News, daktari wa Yanga, Edward Bavu amesema Yondani alipata majeraha ya mkono ambayo anadhani si makubwa sana lakini alitaka mchezaji huyo apumzike walau wiki mbili nje ya uwanja.

" Yondani ameumia lakini si majeraha makubwa sana lakini nilihitaji apumzike walau kwa wiki mbili hivi," amesema Bavu.

Kuumia kwa Yondani ndani ya Yanga kunaongeza idadi ya majeruhi na kufikia wachezaji nane wa kikosi cha kwanza.

Wachezaji wengine ambao wapo nje kwa majeruhi ni Pappy Tshishimbi, Patrick Sibomana, Lamine Moro, Paul Godfrey, Mohamed Isaa, Rafael Daud, Sadney Urikhob.

Imeandaliwa na Rahim Mohamed