Juma Kaseja: Sijawahi Kufundishwa Kudaka Penati.

9th September 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania -Mlinda lango wa timu ya taifa ya Tanzania, Juma Kaseja "Tanzania One" amesema kuwa katika kipindi chake cha miaka 19 ndani ya mpira wa bongo hakuna kocha aliyewahi kumfundisha kudaka penati. Kaseja ameyasema hayo ikiwa ni muda mfupi baada ya kufanikiwa kuisaidia Stars kwaondosha Burundi kwa njia ya matuta na kusonga mbele kwenye hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza kombe la dunia Qatar 2022. Mchezo huo uliofanyika kwenye dimba la taifa, Dar es salaam ambao umeshuhudiwa na mashabiki lukuki waliojitokeza, ulimalizika kwa sare ya 1-1 baada ya dakika 120 ikiwa ni sawa na matokeo ya mchezo wa mzunguko wa kwanza nchini Burundi na ndipo changamoto ya mikwaju ya penati ilipochukuwa nafasi ili kuwatenganisha miamba hao. Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michel walifunga penati zao kwa ustadi mkubwa lakini ilimbidi Kaseja kufanya utundu wake langoni kuhakikisha tuna songa mbele baada ya kupangua mkwaju wa Ngando Omar huku Saidio Berahino na Gigirimana Gael wakitoa nje wenyewe na kuifanya Stars kuibuka na ushindi wa 3-3. "Nadhani hiki ni kipawa tu nilichobarikiwa na Mungu, binafsi sijawahi kufundishwa kudaka penati tangu nilioanza kucheza ligi kuu Tanzania Bara miaka 19 iliyopita," amesema Kaseja anayedakia KMC kwasasa. Kenya vs Stars Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Kaseja kuiokoa Stars kwenye mikwaju ya penati kwa kipindi cha chini ya miezi miwili. Mwanzo mwa mwezi wa nane mlinda lango huyo aliibuka shujaa wakati Stars ilipocheza na Kenya kwenye mchezo wa kufuzu kombe la Chan ambapo alipangua mikwaju miwili ya penati ndani ya dimba la Moi Kasarani na kufanikiwa kufuzu kwa hatua inayofuata. Hata hivyo hiyo imekua ni moja kati ya rekodi zake bora pindi linapokuja suala la penati kwani katika vitu ambavyo mashabiki wa soka nchini hawawezi kusahau ni namna Kaseja alipoweza kucheza mikwaju ya penati ya wachezaji wa Zamaleck na kufanikiwa kuwaondosha kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 2003. Ngo'ombe hazeeki maini Katika hali ambayo iliwaacha mashabiki wengi vinywa wazi ni uamuzi wa Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Ettien Ndayiragije alipoamua kumuita Kaseja kwenye timu ya taifa na kumpa unahodha wakati wa kuelekea mchezo wa kufuzu Chan dhidi ya Kenya. Wengi walishangazwa na uamuzi ule na wengine waliona kuwa amembeba kwa kuwa alikuwa ni mchezaji wake wakati walipokuwa wote KMC. Hata hivyo msemo maarufu unaosema Ng'ombe hazeeki maini ulianza kwendana na uhalisia baada ya mechi mbili dhidi ya Kenya na ilipofika wakati huu wa mechi dhidi ya Burundi maswali kuhusu uwezo wa mlinda lango huyo yalianza kupungua. Kaseja amecheza Simba kwa mafanikio makubwa tangu aliposajiliwa mwaka 2001, hata hivyo mbali na Wekundu hao wa msimbazi, kipa huyo pia amepita Yanga, Azam, Kagera Sugar na sasa yupo KMC. Aibuka na donge la milioni 10 Baada ya kufanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya Burundi, Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amemuahidi Kaseja donge nono la shilingi milioni 10 kama kifuta jasho. "Kwakweli Mungu anazidi kutuonyesha upendo wake, hongera watanzania, hongera Taifa Stars, Kama tulivyoongea jana usiku pale hotelini wachezaji wote mmetimiza kiapo chenu cha jana na mimi naomba muda wenu nitimize kiapo changu kwenu. Mwisho kila mchezo una nyota naomba nimpatie shilingi milioni 10 ndugu yetu Juma Kaseja kama nyota wangu wa leo," umesomeka ujumbe huo wa Makonda kwenye akaunti yake ya mtandao wa Instgram. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya