International Break: Mambo Makubwa 5 Tuliyojifunza Kwenye Mapumziko Ya Mechi Za Timu Za Taifa

16th October 2019

KYIV, Ukraine- Baada ya takribani wiki moja ya mishe mishe ya timu za taifa hatimaye sasa wanchezaji watarudi kwa ajili ya kuendelea na majukumu mengine kwenye klabu zao.

Netherlands
Netherlands
SUMMARY

Baadhi ya rekodi zimevunjwa lakini kubwa zaidi inayoongelewa sana na ambayo itasimuliwa zaidi ni ya mtaalamu kutoka Ureno, Cristiano Ronaldo ambaye kupitia mechi za kimataifa amefanikiwa kufunga bao lake la 700 kwenye maisha yake ya soka.

Kwa wiki hii nzima ingawa hatukufanikiwa kuziona klabu zetu pendwa zikicheza lakini hata kama ulifuatilia ratiba ya mechi za kimataifa naamini kwamba haukujuta kwani kulikuwa na mambo mengi ya kuvutia.

Baadhi ya mambo hayo ni kama haya ambayo yameandaliwa kwenu na mwandishi wa SportPesa News.

Majeruhi

Katika vitu vya kusisimia vilivyotokea kwenye mechi za kimataifa moja wapo ni suala la wachezaji baadhi kuumia.

Wapo waliopata tu majeraha madogo lakini wapo walioumia kwa ukubwa kiasi kwamba kuzitia hofu timu zao za klabu hadi hivi sasa.

Mshambuliaji tegemeo wa PSG, Neymar Jr amepata majeraha akiwa na timu yake ya Brazil na tayari tumeelezwa kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitatu.

Kama hiyo haitoshi, Alexis Sanchez wa Inter Milan naye aliumia akiwa na Chile na taarifa za awali zinasema kuwa huenda akawa nje ya uwanja kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu na kisichozidi miezi minne.

Taarifa nyingine mbaya kwa wapenzi wa Manchester United ni kwamba mlinda lango wao namba moja David de Gea akiwa kwenye jezi ya Hispania amepata maumivu ya nyama za paja na bado haijajulikana atakuwa nje hadi lini kipindi hiki ambacho wanajiandaa kuvaana na Liverpool wikiendi ijayo.

Wachezaji kama Ng'olo Kante, Daniel James wote walipata majeraha kipindi cha mechi za kimataifa lakini inaelezwa kuwa hali zao siyo mbaya sana kwasasa.

Ubaguzi

Tabia mbaya ya ubaguzi kwenye baadhi ya michezo ilijitokeza lakini kubwa zaidi ilikuwa ni kwenye mchezo baina ya Bulgaria waliokuwa wakiwakaribisha Uingereza.

Kwenye mchezo huo, Bulgaria wakiwa nyumbani walipokea kipigo cha 6-0 lakini baadhi ya mashabiki wao walikuwa wakiendekeza tabia mbaya ya ubaguzi majukwaani kiasi cha mchezo huo kusimamishwa mara mbili kwenye kipindi cha kwanza.

Suala hilo limefika mbali zaidi kiasi cha kumkera Waziri Mkuu wa Bulgaria, Boyko Bosissov ambaye bila kufanya ajizi alimtaka rais wa shirikisho la soka nchini humo, Borislav Mihaylov kujiuzulu na yeye akatekeleza agizo siku ya Jumanne.

Timu 6 Za Fuzu Euro 2020

Kwenye maeneo mbalimbali duniani kote kulikuwa na mechi za aina tofauti, nyingine zilikuwa za kirafiki, wengine walikuwa wanagombea kufuzu kombe la dunia nk.

Barani ulaya timu za taifa zilikuwa zikigombea kufuzu Euro 2020. Katika hatua hii waliyofikia tayari kila timu imebakiza mechi mbili ambazo zitamalizwa kwenye breki ijayo ya timu za taifa.

Hata hivyo kwenye mzunguko huu baadhi ya timu zimefanikiwa kujikatia tiketi zao za mapema. Nchi ya kwanza ilikuwa ni Ubelgiji lakini ikafuatiwa na Urusi, Italia, Poland, Ukraine na sasa Hispania nao wamefuzu kwenye mechi yao waliyocheza usiku wa kuamkia leo.

Vipigo Vitakatifu

Kwenye mechi hizi pia tumeshuhudia baadhi ya timu zikiibuka na ushindi mnono huku kinyume chake kikiwa ni baadhi ya timu pia zimekumbana na vipigo vitakatofu.

Ubelgiji ndiyo walioongoza kwenye sekta hii baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa 9-0 dhidi ya San Marino kwenye mchezo uliofanyika mwisho wa wiki iliyopita.

Mbali na Ubelgiji lakini Uingereza pia waliibuka na ushindi mnono wa 6-0 ugenini dhidi ya Bulgaria.

Matokeo hayo ni makubwa zaidi ukilinganisha na matokeo kwenye mechi nyingine.

Rekodi Zavunjwa

Baadhi ya rekodi zimevunjwa lakini kubwa zaidi inayoongelewa sana na ambayo itasimuliwa zaidi ni ya mtaalamu kutoka Ureno, Cristiano Ronaldo ambaye kupitia mechi za kimataifa amefanikiwa kufunga bao lake la 700 kwenye maisha yake ya soka.

Mabao hayo ni mchanganyiko wa timu ya klabu na taifa lakini kizuri ni kwamba bao hilo amefunga wakati akiwa na timu ya taifa kwahiyo nayo imekuwa moja kati ya hadithi za kusisimua ambayo imenilazimu kuiweka hapa.

Kwasasa Ronaldo ameingia kwenye anga la binadamu watano tu duniani ambao katika maisha yao ya soka wamefunga mabao 700 na zaidi nao si wengine bali ni Josef Bican, Romario, Pele, Gerd Mullar na Ferenc Puskas.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya