Hizi Hapa Rekodi Za Bastian Schweinsteiger Baada Ya Kutangaza Kustaafu

9th October 2019

CHICAGO, Marekani- Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani na klabu ya Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger ametangaza kuachana na soka la ushindani mwisho wa msimu huu akiwa na umri wa miaka 35.

Bastian Shweinsteiger
Bastian Shweinsteiger
SUMMARY

Kiungo huyo ameanza kucheza timu ya taifa mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 20 ambapo amefanikiwa kupata nafasi kwenye michezo 121 na kufunga mabao 24 huku pia akiwa ni sehemu ya kikosi kilichoshinda kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Kwasasa Ancheza Chicago Fire inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Marekani klabu aliyojiunga nayo mwaka 2017 akitokea Manchester United.

Zifuatazo ni rekodi zake muhimu kwenye maisha yake ya soka akiwa na timu mbalimbali kama zilivyoandaliwa na dawati la SportPesa News.

Bayern Munich

Schweinsteiger alijiunga Munich kwa mara ya kwanza mwaka 1998 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 14 na moja kwa moja alijiunga na timu ya vijana. Alisajiliwa hapo akitokea TSV 1860 Rosenheim timu ambayo aliitumikia tangu akiwa na umri wa miaka minne.

Kiungo huyo alianza kuitumikia timu ya Munich kikosi cha wakubwa mwaka 2002 akiwa na umri wa miaka 18 na tangu hapo alifanikiwa kucheza mechi 342 akifunga mabao 45 ndani ya miaka 13.

Mwaka 2015, Schweinsteiger alipewa ruhusa ya kuondoka kwenye kikosi hicho na aliyekuwa kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola ambapo alijunga na Manchester United chini ya kocha Louis van Gaal.

Ndani ya Bayern Munich ameshinda mataji 19 kwa ujumla, Bundesliga 8, DFB Pokal 7, DFB Ligapokal 1,  DFB Supercopa 1, UEFA 1.

Manchester United

Akiwa Manchester United, kiungo huyo amefanikiwa kucheza michezo 18 na kufunga bao 1 ndani ya msimu mmoja na nusu kabla ya kuondolewa na kocha Jose Mourinho ambaye alirithi mikoba ya Van Gaal.

Akiwa Man United amefanikiwa kushinda taji la FA chini ya kocha Louis van Gaal.

Chicago Fire

Mwaka 2017, Schweinsteiger alihamia kwenye ligi kuu ya soka nchini Marekani ambapo alijiunga na timu ya Chicago Fire na tangu hapo amecheza mechi 85 huku akifunga mabao 8. Ndani ya klabu hiyo ndipo kiungo huyo ametangaza kuachana na soka ifikapo mwisho wa msimu.

Timu Ya Taifa 

Kiungo huyo ameanza kucheza timu ya taifa mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 20 ambapo amefanikiwa kupata nafasi kwenye michezo 121 na kufunga mabao 24 huku pia akiwa ni sehemu ya kikosi kilichoshinda kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Pia amewakiisha kwenye timu za madaraja yote ya umri kuanzia U16 hadi U21 ambapo kwa ujumla amecheza mechi 26 na kufunga mabao 6.

Tuzo Binafsi

Schweinsteiger ameshinda tuzo binafsi 15 kwenye michuano mbalimbali alipowakilisha timu ya taifa ya Ujerumani, Bayern Munich na Chicago Fire. Hakufanikiwa kushinda tuzo akiwa na Manchester United.

Familia

Tofauti na wanasoka wengi ambao wamekuwa wakijihusisha kwenye mahusiano ya mapenzi na wanamitindo, Schweinsteiger amefunga ndoa na mwanamimichezo ambaye ni mchezaji wa tenesi Ana Ivanovic ambapo wawili hao walioana mwaka 2016 na wana watoto wawili wa kiume (Luka na mwingine ambaye jina lake bado halijajulikana aliyezaliwa miezi miwili iliyopita).

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya