Hii Hapa Timu Ya Wiki Kwenye Michuano Ya Kombe Dunia La Rugby Japan

9th October 2019

TOKYO, Japan- Michuano ya kombe la dunia Rugby inaendela kwa kasi nchini Japan ambapo timu zinachuana vikali kuwania kutinga kwenye hatua ya robo fainali.

Rugby
Rugby
SUMMARY

Ikiwa mzunguko wa mwisho unakaribia kufika tamati mwisho wa wiki hii, kifuatacho ni kikosi cha wachezaji waliofanya vizuri kwenye hatua ya makundi.

15. Stuart Hoggs (Scotland)

Stuart Hoggs amekuwa bora sana kwenye michuano hii hasa wakati timu yake inacheza dhidi ya Samoa. Uimara wake kwenye kuzia ni moja kati ya vitu ambavyo vinamfanya kuwemo ndani ya kikosi hiki.

14. Cheslin Kolbe (Afrika Kusini)

Kolbe ameonesha kuwa ni mchezaji wa kutumainiwa ndani ya timu ya Afrika Kusini. Alikuwa kwenye kiwango cha kukata na shoka wakati timu yake inaibuka na ushindi dhidi ya Italia.

13. Virimi Vakatawa (Ufaransa)

Vakatawa alikuwa na mchezo bora sana dhidi ya Tonga, muda wote wa mchezo alikuwa bize kuhakikisha hakuna kitu kinachoharibika. 

12. Anton Lienert-Brown (New Zealand)

Kwenye mchezo dhidi ya Afrika Kusini, Anton alikuwa bora wakati wakuzuia lakini pia alikuwa na umuhimu mkubwa katika kusambaza mipira huku yeye mwenye akifanikiwa kufunga mara mbili na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi kwenye mechi zote hadi sasa.

11. Semi Radradra (Fiji)

Winga huyo alikuwa kwenye kiwango bora wakati Fiji wakicheza dhidi ya Georgia. Kiwango alichoonesha winga huyo kimenifanya hata kuwaacha nje mawinga Alivereti Raka na Lomano Lemeki ambao nao walikuwa bora sana kwenye michezo yao.

10. George Ford (Uingereza)

Uwezo wa Ford aliouonesha dhidi ya Argentina ni kitu pekee ambacho kinaweza kumshawishi mtu yeyote kumjumuisha ndani ya kikosi hiki cha wiki.

Alikuwa ni kiungo muhimu aliyekuwa akipokea mipira na kuisambaza kwenye maeneo yote ya uwanja kiasi cha viungo wa Argentina kushindwa kabisa kumdhibiti.

9. TJ Perenera (New Zealand)

Amefunga alama muhimu wakati timu yake ikicheza mechi mbalimbali za hatua ya makundi. Uwezo alioonesha wa kuwalamba chenga walinzi wa timu pinzani ni kitu ambacho kimestaajabisha wengi.

1. Siegfried Fisi'ihoi (Tonga)

Mlinzi wa Ufaransa, Sofiane Guitoune alila na viatu baada ya kukabiliana ana kwa ana na Siegfried, jamaa alikuwa anasumbua sana kwenye eneo la kiungo na usiombe utokee mpira wa adhabu ndiyo utajuka kabisa.

2. Mbongeni Mbonambi (Afrika Kusini)

Ingawa watu wengi walitarajia kuwa Afrika Kusini watatawala michuano hii lakini mambo yamekwenda tofauti. Hata hivyo suala hilo halijamfanya Mbonambi kushindwa kuonesha uwezo wake.

Amekuwa na utulivu pindi anapokuwa ameshika mpira na amekuwa ni mmaliziaji mzuri kama tulivyozoea kumuona kwenye michuano mbalimbali.

3. Kyle Sinckler (Uingereza)

Amekuwa akivutia sana ukimtazama wakati wa mapigo ya mipira iliyokufa, walinzi wengi wamekuwa wakishindwa kudili naye.

4. Lood de Jager (Afrika Kusini)

Anahaha uwanja mzima unamkuta yeye si kwenye ulinzi wala kwenye ushambuliaji, ukiangalia kwa wasiwasi huwezi kujua anacheza nafasi gani uwanjani.

5. Jonny Gray (Scotland)

Anafanya kazi kubwa na ya ziada kuhakikisha timu yake inakuwa katika utulivu unaohitajika. Hadi sasa amefanya tackle 13.

6. Rhys Ruddock (Ireland) 

Akiwa kama mchezaji mzoefu ndani ya kikosi amekuwa akifanya kazi kubwa kuhakikisha timu yake haipoteani na ndiyo maana hadi sasa wamefanikiwa kukalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A.

Amekuwa muhimu kwenye idara ya ulinzi sambamba na hilo lakini pia amefunga baadhi ya pointi muhimu sana kwenye michuano hii.

7. Sam Underhill (Uingereza)

Uwezo mkubwa kwenye idara ulinzi akifanya tackling kwenye kila eneo na amekuwa akivunja mashambulizi ya timu pinzani kwa ufasaha sana bila kufanya rafu.

8. Kazuki Himeno (Japan) 

Akiwa ni mchezaji pekee kwa wenyeji kuingia kwenye kikosi hichi lakini hajaingia kwa bahati mbaya bali ni kazi ya kubwa kwenye idara ya unyang'anyaji wa mipira kwa upande wa Japan ndiyo iliyomfanya awepo hapa.

Uwezo wake wa kuiweka Japan salama kwenye idara ya ulinzi ndiyo uliowafanya wenyeji hao wa michuano hii kuwa vinara wa kundi A hadi muda huu.


Imeandaliwa na Badrudin Yahaya