Formula One: Ajali Nyingine Yatokea Mashindano Ya Italian Grand Prix, Mclaren Wakiibuka Kidedea

6th September 2019

ROMA, Italia -Ikiwa ni siku tano tangu kifo cha dereva wa Formula 2, Anthoine Hubert wakati wa michuano ya Belgium Grand Prix kilichotokana na ajali, leo tena imetokea ajali nyingine iliyowahusisha madereva Kimi Raikkonen wa kampuni ya Alfa Romeo na Sergio Perez wa SportPesa Racing Point. Ajali hiyo imetokea wakati wa mazoezi ya kupasha moto kuelekea michuano ya Italian Grand Prix. Hata hivyo hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza kwenye ajali hiyo na madereva wote wapo tayari kwa ajili ya mashindano. Katika mazoezi hayo, dereva wa kampuni ya Ferrari ambaye pia ni bingwa wa michuano iliyomalizika ya Belgium Grand Prix, Charles Leclerc amemaliza kidedea akimzidi dereva wa Mclaren, Carlos Sainz kwa sekunde 0.306. Dereva mwingine wa Mclaren, Lando Norris amekamata nafasi ya tatu akimzidi dereva wa Mercedes, Lewis Hamilton. Hamilton amefanyiwa figisu kali na Sebastian Vettel ambaye hakuwa na kasi lakini aliamua kumfanyia karaha tu. Kwenye mazoezi hayo Vettel amemaliza kwenye nafasi ya nane. Kifo cha Hubert Madereva mbalimbali walioshiriki mashindano ya Belgium Grand Prix walikiri kuwa kifo cha Hubert kilikuwa ni wingu zito kwao wenyewe binafasi lakini pia hata na familia zao. Dereva Lando Norris wa Mclaren alikiri kuwa baba yake aliingia woga na ilimbidi amuhakikishie kuwa atashindana bila ya kupata madhara. "Ilibidi nikae na baba yangu na nimueleze kwa kirefu, kiukweli aliingia uoga lakini nashukuru alinielewa na akaniomba niweze kumaliza salama bila madhara," amesema. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya