Formula 1: Lewis Hamilton Awatia Kiwewe Madereva Wa Ferrari

7th September 2019

ROMA, Italia -Licha ya kuibuka na ushindi kwenye hatua mbili za mazoezi ya awali kabla ya michuano ya Italian Grand Prix, bado madereva wa kampuni ya Ferrari, Charles Leclerc na Sebastian Vettel hawana imani ya ushindi baada ya kuhisi upinzani mkali kutoka kwa dereva wa kampuni ya Mercedes, Lewis Hamilton. Leclerc ambaye ni mshindi wa Belgium GP iliyomalizika hivi karibuni anapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Italian GP na tayari ameshaanza makeke kwenye hatua za kupasha moto baada ya kuongoza katika sesheni zote mbili za mazoezi. Hata hivyo ushindi alioupata si wakuridhisha sana kwani katika awamu ya pili ya mazoezi amemzidi Hamilton kwa sekunde 0.068 kitu ambacho kinawatia hofu timu nzima ya Ferrari kueleka michuano hiyo. Dereva mwengine wa kampuni ya Ferrari ambaye ni bingwa wa duniani Vettel ameshika nafasi ya tatu. "Ni vizuri kushinda kwenye hatua za awali lakini kiukweli kabisa ushindi huu hautoi picha halisi ya jinsi ushindani utakavyokuwa, nategemea Mercedes watakuwa imara kwenye michezo inayofuata," amesema Leclerc. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya