FIBA: Ni Vita Kati ya Argentina Na Spain; Nani Kuibuka Mfalme Mpya Wa Kikapu Duniani Leo?

15th September 2019

BEIJING, China -Fainali ya michuano ya dunia ya mpira wa kikapu inatamatishwa usiku wa leo ambapo miamba ya Marekani ya Kusini, Argentina watavaana uso kwa uso dhidi ya wababe wa Ulaya, Spain

Hispania
Hispania
SUMMARY

Spain unaweza kusema kuwa wana bahati nzuri pindi wanapokuwa wanacheza barani Asia kwani taji lao la mwisho walilichukua kwenye ardhi ya Japan, mwaka 2006.

BEIJING, China -Fainali ya michuano ya dunia ya mpira wa kikapu inatamatishwa usiku wa leo ambapo miamba ya Marekani ya Kusini, Argentina watavaana uso kwa uso dhidi ya wababe wa Ulaya, Spain kwenye mchezo unaotarajiwa kuwa na vuta nikuvute ya aina yake.

Argentina watakuwa wanacheza fainali yao ya kwanza baada ya miaka 17 huku Spain wao watakuwa wanacheza kwenye hatua hiyo baada ya miaka 13.

Timu zote zinaelewa raha ya kubeba taji hilo mbele ya umati wa mashabiki nikiwa na maana kuwa timu zote zimeshawahi kubeba taji hilo. Argentina kwa upande wao walifanya hivyo mwaka 1950 huku wapinzani wao Spain wakiwa wamefanya hivyo mara ya mwisho 2006.

Spain unaweza kusema kuwa wana bahati nzuri pindi wanapokuwa wanacheza barani Asia kwani taji lao la mwisho walilichukua kwenye ardhi ya Japan, mwaka 2006.

Hadi wanafika kwenye hatua hii, Spain wamepita vizingiti kwenye miji ya Guangzhou, Wuhan na Shanghai hadi sasa wanafika Beijing kwenye mchezo wa fainali.

Kwa upande wao Argentina wao wameruka viunzi kwenye miji ya Wuhan, Foshan na Donghuan na wapo tayari kufanya vizuri zaidi ya walivyofanya mwaka 2002 ambapo walifika fainali lakini wakafungwa na FR Yugoslavia.

Washambuliaji Wanashinda mchezo, Walinzi Wanashinda Taji

Spain wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na rekodi nzuri kwenye safu yao ya ulinzi ukilinganisha na timu nyingine. Sergio Scariolo pamoja na wenzie wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya ulinzi na hiyo imekuwa ni kama kawaida ya Spain kwani hata waliposhinda taji Japan walikuwa na idara bora ya ulinzi.

Lakini ni jambo la kusubiri kuona kama walinzi hao wataweza kwenda jino kwa jino dhidi ya mkongwe Luis Scola ambaye licha ya umri wake wa miaka 39 amekuwa na msaada mkubwa kwa timu yake katika kusaidia upatikanaji wa alama nyingi za ushindi.

Scola akishirikiana na Facundo Campazzo na Nicolas Laprovittola wamekuwa wakipasiana vizuri na kusaidia kuwafungua wapinzani ambao wamekuwa wakishindwa kuzisoma mbinu zao.

Facundo Campazzo v Ricky Rubio

Campazzo amekuwa kiungo muhimu kwa Argentina akiwa na msaada mkubwa kwenye kufunga na kutengeneza pointi kwa wenzake na kuelekea mchezo huu atatarajia upinzani mkali kutoka kwa walinzi wa Spain. Kama atafanikiwa kuwashinda walinzi hao basi Argentina watakuwa na mechi nzuri.

Kwa upande wa Rubio yeye ndiyo amekuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Spain, ana wastani wa point 15.9 kwa kila mchezo na wastani wake wa asisti ni 6.4, hicho ni kiwango kizuri kinachomaanisha jamaa yupo kwenye ubora wake wa hali ya juu kwenye michuano hii.

Kinyago Ulichokichonga Hakikutishi

Spain watakuwa wanajivunia kitu kimoja kizuri kwani katika kikosi cha Argentina kinachoshiriki michuano hii, wachezaji 8 wanacheza ligi ya kikapu ya Spain na unaweza ukamuhesabu Scola ambaye naye amecheza nchini humo kwa misimu nane kabla ya kuondoka.

Kwa maana hiyo ni kwamba Spain wanayofaida ya kusema kuwa wachezaji hao wamewazalisha wenyewe na hivyo hawawezi kuwatisha kwenye mchezo wa leo.

Wanavyosema Makocha

"Tuna kikosi mchanganyiko cha vijana na wakongwe, mchezo wa leo utakuwa mgumu kwa pande zote mbili lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri ili kuweza kuwapa furaha mashabiki wetu duniani kote," amesema Sergio Scariolo kocha mkuu wa Spain.

"Tumeshawahi kucheza mechi nyingi dhidi ya Spain, najua wao wanatuheshimu na sisi pia tunawaheshimu sana, mechi itakuwa nzuri yenye ushindani lakini nahisi itakuwa ni fainali ya tofauti na nyingine," amesema Sergio Hernendez kocha mkuu wa Argentina.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya