FIBA: Hispania Watwaa Ubingwa Wa Dunia Wa Kikapu Baada ya Kuiburuza Argentina Kwenye Fainali

16th September 2019

BEIJING, China -Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Hispania imefanikiwa kutwaa taji la dunia la mchezo huo kwa kuwafunga Argentina kwa vikapu 95-75 kwenye mchezo mkali wa fainali uliofanyika usiku wa kuamkia leo.

FIBA
FIBA
SUMMARY

Ubingwa huo inakuwa ni wa kwanza kwa Spain baada ya miaka 13 kupita wakiwa wamechukua ubingwa huo mara ya mwisho mwaka 2006

Shukran za pekee ziwaendee walinzi wa Hispania ambao waliweza kudhibiti njia zote za washambuliaji wa Argentina wakiongozwa na mkongwe Luis Scola ambaye aliwekwa chini ya usimamizi mkali kitu kilichomfanya ashindwe kabisa kufurukuta na kuisaidia timu yake.

Mchezaji nyota wa Hispania, Ricky Rubio amefunga vikapu 20 huku pia wenzake waliofanya vizuri kwenye upande wa ufungaji kwenye timu yao wakiwa ni Rudy Fernandez, Marc Gasol, Sergio Llull.

Kwa upande wa Argentina wachwzaji waliojaribu kufurukuta licha ya kushindwa kuiepusha timu yao na kipigo ni Nikolas Laprovittola aliyefunga vikapu 17 na Gabriel Deck aliyefunga 24.

Hispania wameshinda mchezo huo baada ya kutawala kwenye robo zote nne za mchezo kuanzia na robo ya kwanza ambapo waliibuka na uongozi wa vikapu 23-14, kwenye robo ya pili matokeo yalikuwa ni 20-17, huku robo ya tatu mambo yakiwa 23-16.

Robo ya nne na ya mwisho ilikuwa ngumu zaidi kwa timu zote lakini bado mambo yaliwaendea vizuri Hispania ambapo walimaliza na ushindi wa 29-28 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 95-75.

Hadi mchezo huo unafika nusu ya kwanza kulikuwa na tofauti ya alama 12 ambazo zilikuwa zinaoneka kuwa zinafikika lakini kumalizika kwa robo ya tatu ndipo shida ilipoanza kuonekana kwa upande wa Argentina ambapo walikuwa wamezidiwa vikapu 22 huku wakiwa wanaingia kwenye robo ya mwisho.

Mchezaji Nyota

Ricky Rubio ndio alikuwa kikwazo kwa Argentina kupata ushindi kutokana na kiwango kikubwa alichoonesha kwenye mchezo huo wa fainali. Amefunga vikapu 20, ametengeneza nafasi tatu na kufanya rebound 7.

Ukiachana na hilo, Rubio pia amefanya kazi ya ziada kumdhibiti kiungo mchezeshaji nyota wa Argentina, Facundo Campozza ambaye amefunga vikapu 11 tu kwenye mchezo huo.

Kwa kiwango hicho, Rubio anakuwa ameweka rekodi mpya ya kutengeneza asisti nyingi kwenye kombe la dunia akimfunika Pablo Prigioni ambaye alifanya hivyo mwaka 1994.

Wanavyosema Makocha

"Nadhani tumecheza mchezo wetu mzuri kama tulivyofanya kwenye michezo iliyopita ndani ya mashindano haya, tumeonesha uimara na tunahitaji kuendelea kama hivi, tumejifunza na tunatarajia kuendelea ili kufika kwenye hatua za juu zaidi," amesema kocha wa Argentina Sergio Hernandez.

"Ninawashukuru wachezaji wangu, wamefanya kazi nzuri, kiukweli nilikuwa ninafikra chanya kabla ya mchezo huu lakini wachezaji wangu walikuwa na hofu dhidi ya wapinzani wetu, tunawaheshimu sana Argentina kwa kuwa ni wapinzani haswaa lakini nafurahi tumeshinda,' amesema Sergio Scariolo.


Imeandaliwa na Badrudin Yahaya