EURO 2020: Ronaldo Atamba Kuvunja Rekodi Ya Mabao Duniani Huku Akiipeleka Ureno Euro

18th November 2019

DUDELANGE, Luxembourg- Mshambuliaji na nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefunga bao moja na kuiwezesha timu yake ya taifa kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Luexembourg ugenini

Cristiano Ronaldo
Cristiano Ronaldo
SUMMARY

Ronaldo sasa amefikisha idadi ya mabao 99 kwenye timu ya taifa na yupo nyuma kwa mabao 10 dhidi ya gwiji wa Iran, Ali Daei ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye timu ya taifa.

DUDELANGE, Luxembourg -Mshambuliaji na nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefunga bao moja na kuiwezesha timu yake ya taifa kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Luexembourg ugenini ushindi ambao umewapa tiketi ya moja kwa moja Euro 2020 kutoka kundi B.

Ureno walihitajika kushinda kwa namna yoyote ili wafuzu na ushindi huo sasa umeshusha presha kwa mabingwa hao watetezi wa michuano ya Euro.

Bao la kwanza la Ureno kwenye mchezo huo limefungwa na Bruno Fernandez dakika ya 39 kipindi cha kwanza. Bao hilo lilidumu hadi kwenye dakika ya 86 ambapo Ronaldo akaongeza bao la pili na kuihakikishia timu yake ushindi mwanana.

Ronaldo sasa amefikisha idadi ya mabao 99 kwenye timu ya taifa na yupo nyuma kwa mabao 10 dhidi ya gwiji wa Iran, Ali Daei ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye timu ya taifa.

Mara baada ya mchezo huo Ronaldo aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kuvunja rekodi hiyo na nyingine zilizopo duniani.

"Rekodi zote zinatakiwa kuvunjwa na mimi nitazivunja,' amesema Ronaldo huku akiwa anaonekana kujiamini sana.

Hata hivyo itambidi Ronaldo kusubiri walau hadi mwezi Machi, mwakani ambapo ndiyo kutakuwa na mechi zijazo za timu za taifa. 

Endapo mshambuliaji huyo anayecheza klabu ya Juventus akifunga bao moja basi atakuwa ni mchezaji wa pili kwa upande wa wanaume duniani kufikisha idadi ya mabao 100 kwenye timu ya taifa.

Uingereza Wanapiga Tu

Kwa upande wao timu ya taifa ya Uingereza ambao tayari walishafuzu tangu wiki iliyopita wao wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kushinda 4-0 ugenini dhidi ya timu ya taifa ya Kosovo.

Kwenye mchezo huo ambao ni wa 1001 kwa timu ya taifa ya Uingereza tangu ilipoanzishwa, mabao yao yamefungwa na Harry Winks, Harry Kane, Marcus Rashford na Mason Mount.

Waingereza licha ya kuwa ugenini lakini walipokelewa kishujaa na wageni wao nchi ya Kosovo ambao bado hawajasahau juhudi zilizofanywa na Uingereza kulikomboa taifa lao kwenye kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1999.

Griezmann Aipa ushindi Ufaransa

Kwenye mchezo wa kundi H, Ufaransa wakiwa ugenini wameondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Albania.

Ushindi huo unamaana kwamba Ufaransa sasa wamemaliza michezo kwenye kundi hilo wakiwa mbele ya Uturuki kwenye nafasi ya kwanza.

Mabao ya mabingwa hao wa kombe la dunia kwenye mchezo huo yamefungwa na Corentin Toliso ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Antoine Griezmann. 

Griezmann naye akafunga bao lake kwenye mchezo huo akimalizia pasi nzuri ya ndani iliyotengenezwa na Leo Dubois.

Mshambuliaji wa Chelsea, Olivier Giroud amegongesha mwamba shambulizi lake wakati wageni wakitafuta mabao mengine kwenye mchezo huo.

Matokeo Mengine

Luxembourg 0-2 Ureno

Bulgaria 1-0 Czech

Kosovo 0-4 Uingereza

Albania o-2 Ufaransa

Andorra 0-2 Uturuki

Moldova 1-2 Iceland

Serbia 2-2 Ukraine

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya