EURO 2020: Mambo 5 Yakusisimua Yaliyotokea Kwenye Mechi Za Kufuzu Euro

20th November 2019

CARDIF, Wales- Mechi za kufuzu Euro 2020 zimekamilika usiku wa kuamkia leo huku tukiwashuhudia timu ya taifa ya Wales chini ya kocha wao Ryan Giggs nao kupenya kwa dakika za jioni.

Raheem Sterling
Raheem Sterling
SUMMARY

Finland itashiriki Euro mwakani ikiwa ni moja kati ya timu zenye idadi ndogo ya raia kwenye taifa lao kwa makadirio ya watu milioni 5.5 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2014.

Mabao mawili ya kiungo anayecheza klabu ya Juventus, Aaron Ramsey yametosha kuwapa ushindi wa 2-0 dhidi ya Hungary na sasa wamemaliza kwenye nafasi ya pili ndani ya kundi  F nyuma ya vinara Croatia ambao walifuzu mapema.

Hata hivyo kwenye mechi ambazo zimekusanya mizunguko miwili tangu wiki iliyopita tumeshuhudia mambo mengi ya kusisimua ambayo mtandao wa SportPesa unakudadavulia matano tu makubwa.

Vipigo Vizito

Kwenye hatua hii kuna timu zimeshinda kwa idadi kubwa sana ya mabao huku kinyume chake ikiwa ni kwamba kuna timu zimefungwa kwa idadi kubwa ya mabao.

Mechi ambayo imetia fora zaidi ni ya Italia ambao wamawakandamiza Armenia kwa jumla ya mabao 9-1 kwenye mchezo uliofanyika Jumatatu.

Mbali na mchezo huo lakini pia ushindi wa Uingereza wa 7-0 dhidi ya Montenegro ni moja kati ya mechi zilizozaa mabao mengi zaidi.

Kuna mechi zaidi ya tatu pia ambazo timu zimeibuka na ushindi wa mabao 6. Hivyo hiyo ni kusema kuwa huu ulikuwa ni mzunguko uliozaa mabao ya kutosha.

Finland Wameandika Historia

Mabao mawili aliyofunga mshambuliaji wa Norwich City, Teemu Pukki dhidi ya timu ya taifa ya Liechtenstein yalitosha kuipa uishindi wa 3-0 timu ya taifa ya Finland na kuwafanya kufuzu Euro kwa mara ya kwanza kwenye maisha yao.

Finland itashiriki Euro mwakani ikiwa ni moja kati ya timu zenye idadi ndogo ya raia kwenye taifa lao kwa makadirio ya watu milioni 5.5 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2014.

Ronaldo Anazidi Kusonga

Nohadha wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefunga mabao manne kwenye mechi mbili alizocheza kwenye ratiba hii iliyopita.

Mabao hayoyamemfanya kufikisha idadi ya mabao 99 akiwa na timu ya taifa na sasa amebakisha mabao 10 kumfikia gwiji wa Iran, Ali Daei ambaye ana mabao 109.

Uingereza Ina Washambuliaji Tishio

Kwenye hatua hii ya mechi za makundi unaweza kusema kuwa walikuwa timu tishio kwenye upande wa kupachika mabao ukilinganisha na timu nyingine zote.

Kwneye mechi zao mbili tu zilizopita wamefunga mabao 11 huku wakiwa hawajaruhusu bao hata moja.

Kwa ujumla kwenye mechi zao 8 za kufuzu wamefunga mabao 37 huku mshambuliaji wao Harry Kane pekee akiwa amefunga mabao 12.

Vigogo Wote Wamo

Tofauti na michuano iliyopita ambapo baadhi ya timu kubwa zilikosekana kama vile Uholanzi.

Msimu huu wa michuano ya Euro tutapata kuwashuhudia vigogo wote wa bara la ulaya. Licha ya timu kama Ureno kuonekana kusuasua katika kutakata tiketi lakini mwisho wa siku tiketi zimepatikana na burudani inategemewa kuwa ni kubwa.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya