EPL: Liverpool Kuvunja Mwiko Wa Miaka Mitano Ndani Ya Old Trafford?

20th October 2019

MANCHESTER, Uingereza- Ligi kuu ya Uingereza inaendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ndani ya jiji la Manchester ambapo timu zenye upinzani na mafanikio makubwa nchini humo Manchester United na Liverpool zitakuwa zikiumana

Klopp na Solskjaer
Klopp na Solskjaer
SUMMARY

Liverpool wataingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na kikosi chao kamili ambacho kimezoeleka kwenye macho ya mashabiki wengi mbele kikiongozwa na Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino.

MANCHESTER, Uingereza -Ligi kuu ya Uingereza inaendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ndani ya jiji la Manchester ambapo timu zenye upinzani na mafanikio makubwa nchini humo Manchester United na Liverpool zitakuwa zikiumana ndani ya dimba la Old Trafford.

Mchezo huo ni wa mzunguko wa tisa na kila timu inawania alama tatu kwasababu zake tofauti.

Manchester United chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer hadi sasa wana alama 9 kibindoni wakiwa kwenye nafasi ya 14 na wanazihitaji alama tatu za leo ili walau kuweza kuwa nyanyua japo kwa nafasi kadhaa juu.

Liverpool wao ni vinara wa ligi hiyo wakiwa na alama 24 baada ya kushinda mechi zao zote nane za awali na leo wanazihitaji alama tatu kutoka kwa Manchester United ili kuweza kujiimarisha kileleni kwa kuongoza kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Manchester City.

Mchezo wa leo ni wa 55 kwa miamba hao kukutana kwenye ligi kuu ya Uingereza tangu ilipoanzishwa.

Kwenye michezo 54 iliyopita Manchester United wamekuwa ni wababe zaidi baada ya kushinda kwa jumla ya michezo 28 dhidi ya 14 ya Liverpool. Michezo 12 imekwisha kwa sare.

Manchester United wamekuwa wababe zaidi wanapocheza Old Trafford kwani wameshinda kwa jumla ya michezo 16 huku michezo 12 wakishinda ndani ya Anfield.

No Liverpool hawana rekodi nzuri ndani ya Old Trafford kwani wameshinda mara tano tu katika mechi zote hizo 54 huku mechi nyingine 9 walizishinda kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Kwenye michezo mitano ya mwisho baina ya miamba hao kila timu imeweza kuibuka na ushindi mara moja huku michezo mitatu ikiisha kwa kugawana pointi.

Mara ya mwisho Liverpool kushinda ndani ya Old Traffordi ilikuwa ni Machi 16, 2014 ambapo walishinda kwa jumla ya mabao 3-0 wakiwa chini ya kocha Brendan Rodgers huku United wakiwa na kocha David Moyes.

Mchezaji pekee wa Liverpool aliyekwepo kwenye mechi hiyo na hadi leo bado yupo ni Jordan Henderson.

Tangu kocha Jurgen Klopp alipoteuliwa kuwa kocha wa Liverpool ameshinda mchezo mmoja tu dhidi ya Man United kwenye mchezo wa msimu uliopita kwenye dimba la Anfield ambapo waliibuka na ushindi wa 3-1.

Man United na Liverpool ni wapinzani wakubwa wa soka la Uingereza lakini pia zikiwa ni timu mbili zilizopata mafanikio makubwa kulinganisha na nyingine.

Liverpool japo kuwa hawajashinda taji la ligi kuu ya Uingereza kwa takribani miaka 29 lakini wameshinda kombe hilo mara 18 wakiwa nyuma ya Man United wenye mataji 20.

Hali Ya Vikosi

Liverpool wataingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na kikosi chao kamili ambacho kimezoeleka kwenye macho ya mashabiki wengi mbele kikiongozwa na Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino.

Pia baada ya kukaa nje kwa wiki kadhaa leo mashabiki wa Liverpool wanaweza kumkaribisha kikosini kipa wao namba moja Allison Becker aliyekuwa majeruhi tangu alipoumia kwenye mchezo wa kwanza wa ligi.

Kwa Upande wa Manchester United wao bado wanakabiliwa na hali ya mbaya ya majeruhi. Kiungo Paul Pogba atakuwa ni mmoja kati ya wachezaji muhimu watakaoshindwa kuingia uwanjani lakini pia kiungo Nemanja Matic hakufanya mazoezi ya mwisho na huenda asiwepo kikosini.

Hali ya kipa David de Degea inaendelea vizuri na huenda akacheza mechi ya leo pia washabiki leo watakuwa na furaha kumkaribisha tena kikisoni mshambuliaji wao Anthony Martial pamoja na mlinzi Aaron Wan-Bissaka.

Uso Kwa Uso

Safu ya ushambuliaji ya Manchester United chini ya Marcus Rashford, Daniel James na Anthony Martial watakuwa na kazi ya ziada kukabiliana na ukuta wa Liverpool uliokuwa chini ya Virgil van Dijk pamoja na wenzake kama vile Alexander Anord, Robertson na Matip.

Pia kwa upande wa Liverpool, Salah, Mane na Firmino itawabidi wafanye kazi ya ziada kupenye ngome iliyochini ya mlinzi ghali duniani Harry Maguire akishirikiana na Victor Lindelof, Wan Bissaka na Ashley Young.

Utabiri wa Vikosi

Manchester United: De Gea, Wan Bissaka, Young, Maguire, Lindelof, McTominay, Perreira, Mata, James, Martial, Rashford

Liverpool: Becker, Anord, Robertson, Matip, Dijk, Fabinho, Henderson, Wijnuldum, Salah, Mane, Firmino


Imeandaliwa Na Badrudin Yahaya