EPL: Alonso Aipa Chelsea Pointi 3 Dhidi Ya Newcastle, Spurs Wakibanwa Mbavu Nyumbani

19th October 2019

LONDON, Uingereza- Bao la kipindi cha pili la mlinzi wa kushoto Marcos Alonso limetosha kuwapa alama tatu muhimu klabu ya Chelsea baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle United.

Marcos Alonso
Marcos Alonso
SUMMARY

Nao Tottenham Hotspurs wamenusurika na kipigo kingine cha aibu nyumbani baada ya kufanikiwa kuchomoa bao kwenye dakika ya 86 na kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Watford timu ambayo bado haijawahi kupata ushindi tangu ligi ianze.

Chelsea iliwabidi wawe wavumilivu hadi ilipotimu dakika ya 73 ambapo vijana hao wa kocha Frank Lampard ndipo walipopata nafasi ya kupitisha mpira nyuma ya mlinda lango Martin Dubravka ambaye alikuwa bora sana kwenye mchezo huo.

Newcastle waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na hali ya kujiamini baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Manchester United kwenye mchezo wao wa ligi uliopita.

Matokeo hayo yanawapeleka Chelsea hadi nafasi ya tatu mbele ya Manchester City ambao watacheza mechi ya usiku na Arsenal ambao mechi yao imepangwa siku ya Jumatatu.

Nao vijana wa kocha Brendan Rodgers, Leicester City wameonekana kuendeleza moto wao ndani ya EPL baada ya hii leo tena kupata ushindi wa kusiimu mbele ya Burnley.

Burnley wakiwa ugenini walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Chris Wood lakini Jamie Vardy alichomoa bao hilo kabla ya Youri Tielemans kuongeza la ushindi na kuwapeleka hadi nafasi ya pili nyuma ya Liverpool.

Ushindi huo ni muhimu kwa Leicester ambao walikuwa wanaadhimisha takribani kipindi cha mwaka mmoja tangu Mwenyekiti wao, Vichai Srivaddhanprabha alipofariki dunia kwa ajali ya Helkopta, Oktoba 27, mwaka jana.

Nao Tottenham Hotspurs wamenusurika na kipigo kingine cha aibu nyumbani baada ya kufanikiwa kuchomoa bao kwenye dakika ya 86 na kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Watford timu ambayo bado haijawahi kupata ushindi tangu ligi ianze.

Hata hivyo matokeo hayo bado ni presha kwa kocha Mauricio Pochettino wa Spurs ambaye kwa siku za hivi karibuni inaonekana mambo yake hayaendi vizuri.

Matokeo mengine

Everton 2-0 West Ham

Aston Villa 2-1 Brighton

Bournemouth 0-0 Norwich City

Chelsea 1-0 Newcastle United

Leicester City 2-1 Burnley

Tottenham 1-1 Watford

Wolves 1-1 Southampton

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya