AFCON 2021: Taifa Stars Yaanza Safari Ya Kundi J Kwa Kishindo

16th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania -Timu ya soka ya taifa ya Tanzania "Taifa Stars" imepambana kutoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya taifa ya Equatorial Guinea kwenye mchezo wa kwanza wa kundi J

Taifa Stars
Taifa Stars
SUMMARY

Ikiwa imekatika dakika moja tu kati ya hizo nne za nyongeza ndipo kiungo Salum Abuubakar "Sure Boy" alipofunga bao safi ambalo lilikuwa likisubiriwa na watanzania takribani milioni 50 duniani kote.

DAR ES SALAAM, Tanzania -Timu ya soka ya taifa ya Tanzania "Taifa Stars" imepambana kutoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya taifa ya Equatorial Guinea kwenye mchezo wa kwanza wa kundi J kuwania kufuzu michuano ya Afcon ya mwaka 2021 nchini Cameroon.

Guinea walianza mchezo kwa tahadhari kubwa na ghafla waliwashtua watanzania wengi waliofurika kwenye uwanja wa taifa kwa kufunga bao la kuongoza mnamo dakika ya 16 mfungaji akiwa ni Pedro Mba Obiang aliyefunga kwa shuti kali lililomshinda kimo mlinda lango Juma Kaseja.

Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya wachezaji wa Stars kuanzisha mashambulizi mengi mfululizo ambapo kama si umakini mdogo basi wangeweza kusawazisha ndani ya kipindi kifupi. Hata hivyo bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Stars walikianza kwa umakini zaidi na kujaribu mashambulizi ya hapa na pale lakini hawakuweza kupenya kwenye ukuta uliokuwa ukiundwa na walinzi wenye vimo vikubwa sambamba na uzoefu wa kucheza soka ulaya.

Mabadiliko Ya Ndayiragije

Baada ya kuona mambo ni mazito, kocha wa Stars, Ettiene Ndayiragije aliamua kufanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa mlinzi wa upande wa kulia Hassan Kessy na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Ditrim Nchimbi.

Mabadiliko hayo yalimfanya aliyekuwa mlinzi wa kati Kelvin Yondani kwenda upande wa kulia na Erasto Nyoni ambaye awali alikuwa akicheza kama kiungo mkabaji kushuka kucheza beki wa kati akisaidiana na Bakari Nondo.

Kwa kiasi kikubwa mabadiliko hayo yaliongeza kasi uwanjani na kwenye dakika ya 68, winga Simon Msuva anayecheza ligi ya Morocco kwenye klabu ya Difaa el Jadid alipachika bao la kusawazisha kufuatia jitihada zake binafsi na kutokata tamaa.

Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya wachezaji wa Stars na mashabiki kuzidi kuwa na hamu na bao la ushindi ambapo mara kwa mara lilionekana litaingia wakati wowote.

Mabadiliko ya kumtoa nje Farid Mussa na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga pia yaliongeza kitu kikubwa uwanjani lakini hadi dakika 90 zinakamilika timu hizo zilikuwa 1-1.

Dakika Za Mauaji

Mwamuzi wa akiba Maria Packuita Cynquela alionesha dakika nne za nyongeza kufidia zile zilizopotea kutoka na harakati za hapa na pale ikiwemo wachezaji wa Guinea kujiangusha kwa makusudi.

Ikiwa imekatika dakika moja tu kati ya hizo nne za nyongeza ndipo kiungo Salum Abuubakar "Sure Boy" alipofunga bao safi ambalo lilikuwa likisubiriwa na watanzania takribani milioni 50 duniani kote.

Bao hilo alilifunga kwa shuti kali ikiwa ni sawa na lile walilofunga Guinea kipindi cha kwanza.

Baada ya bao hilo kulizuka tafrani kubwa ndani na nje ya uwanja Guinea wakilalamika kuwa Stars hawakutumia uungwana kwani kuna mchezaji wao alikuwa chini ameumia.

Tafrani hiyo ilimalizika baada ya makocha wa timu zote mbili, Ndayiragije na Sebastien Migne kuonywa kwa kadi za njano kwa kosa la kushindwa kusimamia wachezaji wao.

Alama 3 Muhimu

Hizi ni alama tatu muhimu sana kwa Stars ambao wana nia ya kufuzu kwenye michuano ya Afcon kwa mara ya pili mfululizo.

Kwenye hatua ya kugombea kufuzu michuano iliyopota, Stars walianza vibaya kwa kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Lesotho kocha akiwa mzawa Salum Mayanga. Jambo hilo lilisababisha ugumu kwenye hatua zilizofuata hadi kufikia kufuzu siku ya mwisho tena kwa kutegemea matokeo ya mchezo mwingine.

Hata hivyo benchi la ufundi pamoja na wachezaji safari hii waliahidi kutorudia makosa kama yale ya awali na hadi hapa naweza kusema wameanza kutimiza ahadia yao kwa vitendo.

Ushindi Wa Pili Mfululizo

Ushindi wa leo walioupata Stars ni wa pili mfululizo tangu kocha Ndayiragoje alipopewa timu. Kabla ya kupata ushindi wake wa kwanza wa ndani ya dakika 90 dhidi ya Sudan ugenini, kikosi cha Stars kilikuwa kimecheza mechi sita bila ushindi.

Ushindi huu pia ni wa kwanza kwa kocha Ndayiragije tangu alipopewa timu kama kocha wa kudumu kwa mkataba wa mwaka mmoja.-

Safari Libya

Baada ya mechi hii, Stars sasa wanaelekea Libya kwa ajili ya pambano la pili ambapo watacheza Novemba 19 dhidi ya wenyeji wao mjini Tripoli.

Matokeo Mengine:

Zimbabwe 0-0 Botswana

Imeandaliwa na Raheem Mohamed