EPL: Nyota Wa Leicester City Watawala Kwenye Timu Ya Wiki Ya SportPesa

29th October 2019 - by Adam Mbwana

LEICESTER, Uingereza- Mzunguko wa 10 wa ligi kuu soka ya Uingereza umekamilika mwisho mwa wiki iliyopita

Raheem Sterling
SUMMARY

Hatimaye Pep Guardiola amempata Lionel Messi mwingine ndani ya Man City. Kijana huyo hadi sasa mchango wake hauwezi kuulinganisha na mchezaji mwingine yeyote ndani ya Etihad. Anafunga na kuasisti kila anapojisikia.

LEICESTER, Uingereza -Mzunguko wa 10 wa ligi kuu soka ya Uingereza umekamilika mwisho mwa wiki iliyopita. Ikiwa leo timu zinaanza kushuka tena dimbani kwa ajili ya Kombe la Carabao, SportPesa News imeona ikuletee japo kwa ufupi wachezaji waliounda timu ya wiki kwa mzunguko huo uliopita.

Tim Krul (Norwich City)

Licha ya kuwa timu yake imepoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya ManchesteR United lakini mkongwe huyo mlinda lango wa Uholanzi, Tim Krul alikuwa nyota wa mchezo huo.

Ameokoa penati mbili zilizopigwa na washambuliaji wa Man United, Anthony Martial na Marcus Rashford lakini pia kama unakumbuka kabla ya kufungwa bao la kwanza na Scott McTominay, Krul aliokoa mpira wa kichwa wa Martial ambao asilimia 99 ulikuwa unaingia kambani.

Aaron Wan-Bissaka (Man United)

Aaron Wan-Bisaka alikuwa ni muhimili wa timu ya Man United kwenye eneo lao la kujilinda. Wikiendi hii amefanya tackling sahihi 11 ambazo ni nyingi kuliko mchezaji yeyote kwenye ligi mzunguko wa 10.

Ben Chilwell (Leicester City)

Ni mmoja kati ya wachezaji waliowapa wakati mgumu sana Southampton siku ya Ijumaa na kusababisha ushindi wa 9-0 kwa timu yake.

Alikuwa akiutumia upande wake wa kushoto kuanzisha mashambulizi mengi, ametoa pasi tatu zilizozaa mabao huku yeye akifunga bao moja ambalo lilikuwa ndiyo la kwanza kwa mchezo.

Jamaal Lascelles (Newcastle)

Jamaal Lascelles ambaye ni mlinzi wa kati na nahodha wa Newcastle alikuwa kwenye kiwango bora wakati timu yake ikipata sare ya 1-1 dhidi ya Wolves.

Aliweza kuokoa mipira ya juu na kuzima mashambulizi yote ya kushtukiza ya Wolves huku akifanikiwa kumdhibiti vilivyo Raul Jimenez.

Sokratis (Arsenal)

Licha ya kuwa timu yao iliweza kufanya uzembe wa kusawazishiwa mabao mawili dhidi ya Crystal Palace lakini kitu pekee cha kujivunia kwa mashabiki wa Arsenal na hali ya kujituma ya mlinzi wao wa kati Sokratis.

Alifunga bao moja la kuongoza na alifunga bao la dakika za majeruhi ingawa lilikataliwa kupitia VAR lakini bado haiepushi ukweli kuwa mchezaji huyo ni moja kati ua usajili mzuri uliofanywa na Unai Emery tangu arithi mikoba ya Arsene Wenger.

Fabihno (Luverpool)

Ukiachana na uzembe uliofanyika hadi kupatikana bao la kwanza la Spurs, Fabinho aliweza kutuliza eneo lote la ulinzi la Liverpool na hadi kufanikiwa kupata ushindi wa 2-1.

Spurs walikuwa na mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza lakini mipango yao mingi ilikuwa inaishia kwa kijana huyu raia wa Brazil.

Christian Pulisic (Chelsea)

Amefunga Hat Trick yake ya kwanza kwenye maisha yake ya soka. Tangu alipojiunga na Chelsea akitokea Borrusia Dortmund kocha Frank Lampard alionekana kumpa muda zaidi wa kuzoea mazingira ya Uingereza.

Mabao matatu aliyofunga yameisaidia timu yake kupata ushindi wa 4-2 ugenini dhidi ya Burnley na huenda ndiyo ukawa mwanzo wake wa kuanza kuonesha kile ambacho mashabiki wengi wanakitaraji kutoka miguuni mwake.

Ikay Gundogan (Manchester City)

Ilikay Gundogan amekuwa sio mtu wa kutajwa sana kwenye mafanikio ya Man City lakini nikwambie tu kiungo huyo amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuifanya timu yake iwe bora kwenye kila mchezo.

Dhidi ya Aston Villa aliwekwa eneo la chini akiwalisha mipira, David Silva na Kelvin De Bruyne. Aliifanya kazi hiyo kwa ufasha mkubwa na akamalizia kwa kufunga bao na kuipata timu yake ushindi wa 3-0.

Jamie Vardy (Leiceater City)

Huyu ndiye Jimmy Vardy tunayemjua. Hapa namzungumzia yule Vardy wa mwaka 2026 ambaye alikuwa na kasi na target kubwa golini. Hat Trick yake dhidi ya Southampton imemfanya kuwapiku Tammy Abraham na Sergio Aguero kwenye kinara cha upachikaji wa mabao akifikisha idadi ya 9.

Ayoze Perez (Leicester City)

Mshambuliaji mpya wa Leicester City ambaye taratibu anaanza kuingia ndani ya timu. Amejiunga msimu huu akitokea Newcastle lakini maisha yake ndani ya King Power hayakuanza kwa njia nyepesi.

Hata hivyo mabao aliyofunga ni alamu kwa wachezaji wote ambao wanagombea naye namba ndani ya timu hiyo.

Raheem Sterling (Manchester City)

Hatimaye Pep Guardiola amempata Lionel Messi mwingine ndani ya Man City. Kijana huyo hadi sasa mchango wake hauwezi kuulinganisha na mchezaji mwingine yeyote ndani ya Etihad. Anafunga na kuasisti kila anapojisikia.

Kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa amefunga bao moja hiyo ikiwa ni siku chache tu tangu alipofunga hat trick kwenye mchezo wao wa Ligi ya mabingwa ulaya.

Imeandaliwa na Jery Mlosa