Copa Libertadores: Boca Juniors VS River Plate Ni Derby Ya Visasi, Jasho Na Damu

1st October 2019 - by Adam Mbwana

BUENOS AIRES, Argentina -Alfajiri Ya kuamkia kesho Majira ya saa tisa na nusu kwa saa za Afrika Mashariki pale kwenye mji wa La Boca ndani ya dimba la Estadio Alberto J. Armando kutakuwa na pira la kukata na shoka

Boca Junior
SUMMARY

Kwa kifupi ni kwamba hii ni moja kati ya mechi bora kabisa duniani ambayo imekuwa ikikusanya vituko vya aina yake ndani na nje ya uwanja na mwisho wa yote mpira ambao huwa unapigwa ni wa kiwango cha dunia.

BUENOS AIRES, Argentina -Alfajiri Ya kuamkia kesho Majira ya saa tisa na nusu kwa saa za Afrika Mashariki pale kwenye mji wa La Boca ndani ya dimba la Estadio Alberto J. Armando kutakuwa na pira la kukata na shoka ambapo vigogo wiwili vya soka nchini Argentina na Amerika Kusini kwa ujumla, Boca Juniors watawakaribisha River Plate kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Copa Libertadores.

Timu hizo hasimu uwanjani zenye upinzani wa hali ya juu zitakuwa kwenye mchezo wa kombe hilo ambalo ni sawa na UEFA Champions League au Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wao wa bara la Amerika Kusini.

Mara hii wanakutana kwenye michuano hiyo ikiwa ni miezi tisa tu imepita tangu walipokutana kwenye fainali ya michuano hiyo hiyo iliyogubikwa na utata mkubwa kiasi kwamba ikaamuliwa mchezo mmoja wa fainali ukapigwe kwenye dimba la Santiago Bernabeu nyumbani kwa Real Madrid.

Mchezo ulikuwa kama ifuatavyo

Wababe hao wenye upinzani uliopitiliza na kuhesabika kuwa ni moja kati ya derby zenye uhasama mkubwa duniani walikutana kwenye fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 58. 

Kumbuka fainali ya michuano hiyo kwa Amerika Kusini ilikuwa inachezwa kama ligi ya mabingwa Afrika yaani nyumbani na ugenini lakini kutokana na fujo za wababe hao mwaka jana, Shirikisho la Soka Amerika Kusini limeamua kufanya mchezo wa fainali kuwa mmoja tu ambao utapigwa kwenye uwanja tofauti.

Wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, Boca Juniors walilazimishwa sare ya 2-2. Siku ya mchezo wa marudiano ilipowadia wakati basi lililobeba wachezaji wa Juniors likiwa linaingia uwanjani lilijikuta likishambuliwa sana na washabiki wa River Plate na kuvunjwa vioo vyote na kusababisha wachezaji wengi kuumia akiwemo Carlos Tevez, suala lilipolekea mchezo kughairishwa.

Baada ya majadiliano ya muda fulani ndipo ilipoamuliwa goma lipelekwe Hispania kwenye mji wa Madrid na siku ya mchezo walimwagwa askari utadhani uchafu. 

Hata hivyo pamoja ya kuwa River Plate ndiyo waliosababisha ugomvi walijikuta wakiibuka na ushindi wa 3-1 na kufanikiwa kunyakuwa ubingwa wa michuano hiyo. 

Mchezo huu huwa unavuta hisia za wanasoka wengi duniani hasa wenye asili ya Amerika Kusini, mfano kwenye mchezo uliofanyika Bernabeu nyota maarufu duniani kama vile Lionel Messi na Paul Dyabala walitimba ndani ya uwanja kushuhudia mtanange ingawa wao kwasasa wanacheza vilabu vya ulaya.

Wameshachafuana

Unaambiwa tayari miamba hao wameshacheza mchezo mmoja wa ligi ya Argentina uliopigwa Septemba, 1 na kama ilivyo ada kilinuka kweli kweli.

Wachezaji 10 walioneshwa kadi za njano kwenye mchezo uliojaa vita baina ya wachezaji uwanjani, kitu kizuri ni kwamba nje ya uwanja mambo yalikuwa shwari hasa baada ya timu hizo kushindwa kufungana baada ya kutoka sare ya 0-0.

Kwa kifupi ni kwamba hii ni moja kati ya mechi bora kabisa duniani ambayo imekuwa ikikusanya vituko vya aina yake ndani na nje ya uwanja na mwisho wa yote mpira ambao huwa unapigwa ni wa kiwango cha dunia.

Upinzani wa timu hizi ni mkubwa sana ambao unalinganishwa na ule wa Glasgow Derby ambayo ni Celtic vs Rangers.

Wanapokutana wababe hawa mbali na wachezaji kuvuja jasho uwanjani lakini pia mashabiki kupigana na kulipiziana visasi ni kitu cha kawaida sana na ndiyo maana pindi timu hizo zinapokutana ulinzi unaimarishwa kuliko kitu chochote kile kwani hawachelewi kubadilikiana.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya