Uchambuzi: Kitu Gani Jose Mourinho Atakileta Ndani Ya Tottenham Hotspurs?

21st November 2019

LONDON, Uingereza- Ndoa iliyodumu kwa miaka mitano kati ya kocha raia wa Argentina, Mauricio Pochettino na klabu ya Tottenham Hotspurs imefika tamati kama ilivyobainishwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy usiku wa Novemba 19, 2019.

Jose Mourinho na Harry Kane
Jose Mourinho na Harry Kane
SUMMARY

Kwa ujumla wanacho kikosi kizuri chenye wachezaji bora ambao wanaweza kucheza kwenye timu nyingi barani ulaya lakini suala la uzoefu limekuwa likiwagharimu kwa kiasi fulani.

Kuondoka kwa Pochettino kunako White Hart Lane kumefungua njia kwa kocha mjivuni na mwenye maneno mengi Jose Mourinho kuchukuwa nafasi hiyo kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.

Suala la Pochettino kutimuliwa kazi msimu huu lilikuwa ni la kungojea muda tu kwani mwenendo wa kikosi hicho ulikuwa siyo wa kuridhisha hasa kwenye michezo ya ligi.

Hata hivyo jina la Mourinho kuchukuwa nafasi yake ndiyo jambo ambalo huenda kuwa ni kivutio kikubwa kwasasa kwa wapenda soka duniani kote wakijiuliza ni nini Spurs wanalenga kwasasa kwenye klabu yao.

Mourinho kwa miaka yake takribani 19 akiwa kwenye tasnia ya ukocha wa mpira wa miguu amejipambanua kama mmoja kati ya mameneja bora kabisa akiwa na rekodi za ushindi kwenye timu mbalimbali alizozifundisha.

Amekubali kuifundisha Spurs timu ambayo mara ya mwisho kushinda taji ilikuwa ni miaka 11 iliyopita ambapo walishinda kombe la Carling.

Je ni kitu gani Mourinho atakileta ndani ya klabu ya Spurs kwa miaka miwili na nusu kama atamaliza mkataba wake?

Dhamira Ya Ushindi

Mpende au mchukie lakini Mourinho kama nilivyosema hapo awali ni mmoja kati ya makocha bora na washindi hapa duniani.

Hakucheza mpira kwa daraja la juu lakini tangu alipoanza kazi ya ukocha miaka 19 nchini Ureno hadi kufikia sasa ameshashinda mataji 25.

Mataji hayo ni pamoja na ligi ya mabingwa mawali lakini pia ameshinda EPL tatu akiwa na Chelsea ambayo aliifundisha kwa vipindi viwili tofauti.

Uzoefu

Kwa miaka ya hivi karibuni Spurs wamekuwa wanaonekana kuwa moja kati ya timu bora sana ndani ya EPL. Hapa hatuna budi kusifu kazi nzuri iliyofanywa na kocha Pochettino kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo tatizo kubwa la Spurs limekuwa likionekana kwenye suala zima la uzoefu hasa kwenye dakika za mwisho wa michuano.

Mfano mdogo nikupe kwenye msimu wa 2015-16 wakati Leicester City wanachukuwa taji la ligi, kama Spurs wangekuwa na ile hali ya uzoefu kwa kiasi fulani basi pengine leo hii tungekuwa tunaongea habari nyingine.

Msimu ule Spurs waliwabana Leicester City hadi kwenye mechi za mwishoni kabisa mwa msimu lakini walijikuta wakianza kuputeza michezo muhimu na hadi kufikia kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu.

Kwa ujumla wanacho kikosi kizuri chenye wachezaji bora ambao wanaweza kucheza kwenye timu nyingi barani ulaya lakini suala la uzoefu limekuwa likiwagharimu kwa kiasi fulani.

Ujio wa Mourinho ndani ya kikosi chao itakuwa ni faida kubwa sana kwenye upande wa kukiongezea uzofu kikosi chao.

Safu Bora Ya Ulinzi

Katika vitu ambavyo Mourinho amekuwa akisifiwa navyo zaidi ni suala la kusuka ukuta wa chuma kwenye kila timu alizokuwa anakwenda kufundisha.

Falsafa hiyo ya Mourinho amekuwa akiitumia na imempa mafanikio kwenye timu za Chelsea ambapo kupitia walinzi John Terry na Ricardo Carlvalho alitengeneza safu ya ulinzi iliyompa mataji mawili ya EPL.

Alipokwenda Real Madrid alisuka safu ya ulinzi chini ya Pepe na Sergio Ramos na alipokuwa Inter Milan alitengeneza ukuta wa Walter Samuel na Lucio.

Ndani ya Spurs tutegee kuinua ubora wa Jan Vertonghen, Toby Alderweireld, Davinson Sanchez ambao wanasaidiwa na Tanguy Ndombele na Harry Winks kwenye safu ya kiungo wa ukabaji.

Nafasi Ya Kuthibitisha Ubora Wake

Uhamisho wa kujiunga na Spurs kwa Mourinho umekuja kwa wakati sahihi kipindi ambacho baadhi ya watu walianza kutilia mashaka kuhusu uwezo wake.

Wapo hadi sasa wanaoamini kwamba mbinu za Mourinho zimefika kikomo na haziwezi kufua dafu kwenye kipindi tulichopo kutokana na aina ya mpira unaochezwa kwasasa na hata aina ya wachezaji waliopoa duniani hivi sasa.

Kwahiyo hii ni nafasi ya Mourinho kuwaonesha watu kwamba mawazo hayo ni ya kweli ama si ya kweli kwa upande wake.

Mzee Wa Drama

Mourinho akiwa na umri wa miaka 56 anabaki kuwa mmoja kati ya makocha wenye vituko na vibweka vingi kila anapokwenda.

Wakati anajiunga na Chelsea kwa mara ya kwanza ndiyo alijipachika jina la Special One na aina ya ushangiliaji wake ulikuwa ni moja kati ya vitu vya kuvutia sana.

Pia suala lake la kuchagua kutengeneza vita ya maneno dhidi ya makocha wa timu pinzani ni moja kati ya vitu ambavyo bado vinamzunguka katika maisha yake.

Sidhani kama unaweza kusahau tukio lake dhidi ya kocha marehemu Tito Vilanova wakati huo Mourinho akiwa kocha wa Madrid huku marehemu akiwa msaidizi ndani ya Barcelona.

Hata ndani ya Manchester United alikuwa na drama za hapa na pale dhidi ya uongozi hasa baada ya kushindwa kutekelezewa mahitaji yake ya usajili lakini pia kama unakumbuka alikuwa kwneye mzozo mkubwa dhidi ya Paul Pogba kama alivyofanya dhidi ya Iker Casillas wakati wakiwa Madrid.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya