Kufuzu CHAN: Hivi Ndivyo Washujaa Wetu Walivyojituma Kwenye mechi Ya Sudan vs Taifa Stars

19th October 2019

KHARTOUM, Sudan- Mabao mawili ya mlinzi Erasto Nyoni na mshambuliaji Ditram Nchimbi yametosha kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuibuka na ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Sudan

Taifa Stars
Taifa Stars
SUMMARY

Kama unakumbukwa jina la Nchimbi lilitajwa mwishoni ikiwa ni siku moja baada ya kuwafunga Yanga Hat Trick kwenye mchezo wa ligi kuu.

KHARTOUM, Sudan- Mabao mawili ya mlinzi Erasto Nyoni na mshambuliaji Ditram Nchimbi yametosha kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuibuka na ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Sudan na kufanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN nchini Cameroon mwaka 2020.

Ushindi huo unakuwa ni wa kwanza ndani ya dakika 90 kwa Taifa Stars tangu kocha Etiene Ndayiragije alipochukuwa mikoba ya nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mnigeria, Emmanuel Amunike.

Dawati la SportPesa News ambalo lilikuwa macho kuufatilia mchezo huo mwanzo mwisho limekuja na wastani wa viwango vya wachezaji waliocheza mchezo huo.

Kwanza kabisa ni kocha Etiene Ndayiragije ambaye kwa mechi ya jana bila kificho analamba 90% kutokana na mambo aliyofanya.

Kwanza kumuita Ditram Nchimbi licha ya kuwa hapo awali alikuwa amemuacha, Nchimbi amekuwa kama kamari iliyokwenda sawa kwa kocha huyo raia wa Burundi.

Pili sub ya kumuingiza Chilunda na kumuacha Nchimbi uwanjani. Wengi walitegemea kumuona Chilunda akichukuwa nafasi ya Nchimbi kwa kuwa wote wanacheza nafasi moja ya namba tisa.

Hata hivyo kocha aliaumua kuwaacha wacheze washambuliaji wawili na matokeo yake wakazaa matunda baada ya kushirikiana kufunga bao la pili.

Kwa mantiki hiyo tunamtangaza kocha Ndayiragije kuwa ndiyo nyota wa mchezo wa jana.

1. Juma Kaseja 70%

Kwenye mchezo huo mlinda lango mkongwe nchini Juma Kaseja ameruhusu bao moja ambalo pia huwezi kumtupia lawama moja kwa moja. Bao hilo lilikuwa ni kushindwa kujipanga kwa walinzi pamoja na viungo wa Stars ambao walitoa mwanya mkubwa kwa wa Sudan kutengeneza bao jepesi.

Kwenye maeneo mengine Kaseja alionesha ukongwe na uzoefu wake pale ilipobidi na hata tulipokuwa tunaongoza aliwatuliza wachezaji wenzake hadi mpira unaisha.

2. Salum Kimenya 40%

Amecheza vizuri kwa kiwango chake hasa ukizingatia hana uzoefu na mechi kubwa za kimataifa kama ilie ya jana. Alishindwa kukaba kwa nafasi kwenye tukio ambalo lilisababisha Stars kufungwa bao la kwanza kipindi cha kwanza.

3. Gadiel Michel 60%

Kama kawaida yake alifanya kazi kubwa kwenye kuzuia mashambulizi ya wapinzani yaliyokuwa yanapitia upande wa kushoto lakini pia alikwenda kushambulia na kuungana na Miraj Athuman pale ilpokuwa inabidi.

4. Eraston Nyoni 70%

Kama kawaida yake amekuwa ni mlinzi mwenye utulivu wa hali ya juu licha ya kuwa umri wake umesogea kwa kiasi fulani. Utulivu wa hali ya juu pindi anapokuwa na mpira ndiyo silaha yake kubwa. Bao alilofunga lilikuwa muhimu zaidi na liliweza kuwarudisha wachezaji wenzake mchezoni. 

5. Bakari Nondo 80%

Kukosekana kwa Kelvin Yondani kwenye mchezo huu ilikuwa ni hadithi mbaya ambayo watanzania wengi walikuwa hawatamani kuisikia. Ghafla akaibuka Bakari Nondo na kuja kuziba vizuri nafasi yake kwenye mchezo mgumu wa ugenini. Kiukweli anastahili sifa nyingi sana hasa ukizingatia ule ndiyo mchezo wake wa kwanza wa kimataifa. 

6. Jonas Mkude 70%

Watoto wa mjini wanasema vocha, jana kiukweli tulishuhudia vocha zikitumwa sana na  Jonas Mkude akitokea shimoni kwenye eneo la namba 6. Alikuwa akipokea mipira na kuisambaza vizuri alikuwa anapiga turn za akili kiasi kwamba pale katikati alikuwa anaonekana yeye tu.

7. Miraj Athumani 65%

Licha ya kuwa na ugeni na mechi za kimataifa lakini bado Miraji Athuman "Sheva" hakuonesha uoga hata kidogo. Kila alipopata mipira alijaribu kufanya jambo. Kama unakumbuka Miraj Athuman ndiye aliyekuwa anatembea na mpira akiliekea lango hadi alipofanyiwa faulo ambayo ikazaa bao baada ya kupigwa na Nyomi. Pia alikuwa anasaidia sana kwenye eneo la ulinzi.

8. Frank Domayo 60%

Ukitaja maeneo ambayo Stars walikuwa vizuri huwezi kuliacha eneo la kati, Frank Domayo amefanya kazi nzuri akishirikiana na viungo wenzake.

9. Ditram Nchimbi 75%

Nchimbi ameonesha kuwa ni mshambuliaji mzuri ambaye tulikuwa tunamkosa kwenye michezo iliyopita. Baada ya kuitwa tu kwa mara ya kwanza amefunga bao muhimu lililoipeleka Stars CHAN.

Kama unakumbukwa jina la Nchimbi lilitajwa mwishoni ikiwa ni siku moja baada ya kuwafunga Yanga Hat Trick kwenye mchezo wa ligi kuu.

Bao alilofunga dhidi ya Sudan limeonesha kuwa kweli yeye ni namba tisa mzuri kwani alifuatilia mjengo wa Shaban Chliunda na hadi kukaa kwenye eneo ambalo mpira umekuja na kumalizia mbele ya walinzi wa Sudan.

10. Mzamiru Yassin 70%

Kiungo mgumu mwepesi unaweza kumuita. Ukitaka udambwi upo na ukitaka purukushani zipo. Nini ambacho haukijui kuhusu Mzamiru Yassin? kwenye mchezo wa jana alikuwa kama Invicible akifanya kazi kubwa pale kati iliyofanya maisha yawe mepesi kwa Stars lakini magumu kwa Sudan.

11. Idd Seleman "Nado" 65%

Kila eneo la uwanja unamkuta yeye. Anakimbia kila kona kila idara. Mara hii anapokelea mpira kati mara yupo mbele mara kaja kuokoa. 

Akiba

Shaban Chilunda 70%

Baada ya kuwa katika lawama kwa kukosa mabao mengi kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es saalam, safari hii Chilunda ametokea sub na kufanya mambo mazito. Aliwachukuwa walinzi wa Sudan kwa namna alivyojisikia kabla ya kutengeneza bao la ushindi kwa Nchimbi.

Abuubakar Salum/ Hakuwa na muda wa kutosha uwanjani kuonesha jambo.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya