Kongole: Simba Wamepiga Hatua Moja Mbele Kuelekea Kuwa Klabu Kubwa Afrika

20th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Kama umekuwa ni mfuatiliaji wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii basi katika pitapita zako utakuwa umekutana na taarifa kuhusu klabu ya Simba kuwa mbioni kumalizia viwanja vyao vya mazoezi.

Ujenzi wa Uwanja wa Mazoezi wa Simba
Ujenzi wa Uwanja wa Mazoezi wa Simba
SUMMARY

Kwa namna yoyote ile ninakiri kuwa hatua ambayo wameianza Simba ni hatua kubwa mno na hii sasa ndiyo kusema kuwa wanatimiza kwa vitendo ile nia ya viongozi kutaka timu hiyo kuwa moja kati ya klabu kubwa barani Afrika.

Taarifa hiyo ni bora sana kwa mashabiki wa timu hiyo kongwe hapa nchini ambayo ina umri wa takribani miaka 83.

Kwa kipindi cha miaka yote hiyo tangu ilipoanzishwa timu hiyo haikuwahi kuwa na sehemu yao rasmi walau tu ya kufanyia mazoezi na badala yake walikuwa wakitanga tanga kwenye sehemu tofauti ambazo walikuwa wanalazimika kutumia fedha ili kupata huduma ya kutumia maeneo.

Ingawa jambo hili na naweza kusema kuwa limechelewa lakini ni moja kati ya matukio bora ambaya yataingia kwenye historia ya muda mrefu wa klabu hiyo.

Simba ambao wanadhaminiwa na kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa walianza harakati za ujenzi wa uwanja huo tangu enzi za aliyekuwa Mwenyekiti wao mstaafu Ismail Aden Rage lakini changamoto kubwa inaonekana kuwa ilikuwa ni fedha za kukamilisha kwa jambo hilo.


Sehemu ya Uwanja kabla ya kutandazwa kwa nyasi bandia. (Picha kutoka Simba-Twitter)

Hata hivyo kuingia kwenye mfumo wa uwekezaji chini ya Bilionea, Mohamed Dewji kumeonekana kuongeza chachu na hamasa zaidi ya kulikamlisha jambo hilo ambalo kwasasa naweza kusema limekamilika kwa zaidi ya asilimia 85.

Uwanja huo utaweza kuokoa baadhi ya mapato ya klabu ambayo hapo awali yalikuwa yanakwenda kwenye viwanja mbalimbali vya ndani na nje ya mkoa kwa ajili ya kufanyia mazoezi.

Lakini kama itawapendeza basi eneo hilo linaweza kuja kuzaa uwanja kamili ambao utakuwa ukitumika kwa ajili ya mechi za ligi na hata za kimataifa kitu ambacho sasa kitageukua na kuwa kitega uchumi kikubwa kwa klabu.

Klabu kubwa duniani kote ambazo zimeendelea huwa zinamiliki viwanja vyao binafsi ambavyo hutumika kama msingi wa kwanza kabisa wa mapato ya klabu kabla ya kwenda kwenye vyanzo vingine.

Ndani ya uwanja wanapata wadhamini ambao watasambaza mabango ya matangazo mbalimbali na fedha zote zitakuwa ni za klabu ambao ni wamiliki wa uwanja husika.

Kwa namna yoyote ile ninakiri kuwa hatua ambayo wameianza Simba ni hatua kubwa mno na hii sasa ndiyo kusema kuwa wanatimiza kwa vitendo ile nia ya viongozi kutaka timu hiyo kuwa moja kati ya klabu kubwa barani Afrika.


Sehemu ya Uwanja baada ya kutandazwa kwa nyasi bandia. (Picha kutoka Simba-Twitter)

Ni ngumu sana kushindana na timu kama Kaizer Chief, Al Ahly, TP Mazembe, Etoile du Sahel na Esperience kama hauna hata uwanja wa mazoezi unaomilikiwa na klabu.

Hii ni hatua moja kati ya nyingi ambazo naweza kusema Simba wamepiga wakati wakielekea kuwa moja kati ya timu kubwa barani Afrika.

Hatua hii inapaswa kuigwa na timu nyingine zinazoshiriki kwenye ligi ya Tanzania Bara ikiwa zina malengo ya kufika mbali kimataifa.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya