Formula 1: Charles Leclerc Ashinda Italian GP Baada ya Kumdhibiti Hamilton

9th September 2019

ROMA, Italia -Dereva wa kampuni ya Ferrari, Charles Leclerc ameshinda mbio za Italian Grand Prix baada ya kuwadhibiti ipasavyo madereva wa Mercedes, Valtteri Bottas na Lewis Hamilton. Akiwa katikati ya mashindano, Leclerc, 21 aliamua kudili na Hamilton kwa kumzuia kwa muda kisha kupata upinzani mwingine kutoka kwa Bottas ambaye naye alimshinda na kufanikiwa kumaliza kinara. Wingu zito limetanda mbele ya bingwa mara nne wa dunia ambaye naye ni dereva wa Ferrari, Sebastian Vettel ambaye alifanya kosa kubwa lililomgharimu. Ushindi wa Leclerc ni wa pili mfululizo baada ya kushinda Belgium GP wiki iliyopita na ushindi wa kwanza kwa Ferrari kwenye ardhi ya nyumbani tangu Fernando Alonso alipfanya hivyo mwaka 2010. "Sikuwa nimechoka sana kabla ya kuja kushindana kwenye mbio hizi, yalikuwa ni mashindano magumu zaidi lakini ushindi huu ni ndoto ambayo imetimia kwangu," amesema Leclerc. SportPesa Racing Point Dereva Sergio Perez kutoka imu ya Racing Point inayodhaminiwa na kampuni ya SportPesa, alimaliza katika nafasi ya saba na kujinyakulia jumla ya alama sita huku mwenzake Lance Stroll raia wa Canada akimaliza katika nafasi ya 12 akiwa hajakusanya alama hata moja. Imeandaliwa na Badrudin Yahaya