EPL: Matukio Matano Ya Kusisimua Yaliyotokana Na VAR Msimu Huu

12th November 2019

LONDON, Uingereza- Tangu ilipoanza kutumika kwenye mashindano mbalimbali msimu uliopita VAR imekuwa kwenye mijadala mizito kutoka kwa wadau wa soka huku wengi wakiwa na mawazo tofauti.

VAR
VAR
SUMMARY

Mwamuzi aliambiwa kuwa Aymeric Laporte ambaye ni mlinzi wa Man City aliunawa mpira kabla ya kufika kwa mfungaji na hivyo baada ya kuhakikishiwa kuhusu suala hilo alilifuta bao hilo na mechi ikaisha kwa 2-2.

LONDON, Uingereza -Tangu ilipoanza kutumika kwenye mashindano mbalimbali msimu uliopita VAR imekuwa kwenye mijadala mizito kutoka kwa wadau wa soka huku wengi wakiwa na mawazo tofauti.

Wapo wanaoona ni wakati sahihi kwa soka kutumia teknolojia hiyo na wengine wanaona kuwa bado haikuwa wakati sahihi.

Visanga vya VAR vinajulikana, kuanzia kwenye kombe la dunia mwaka jana huko nchini Urusi hadi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na baadhi ya ligi ambazo zilianza kutumia teknolojia hiyo msimu uliopita.

Nani hakumbuki tukio la Manchester United kuwaondosha PSG kwenye hatua ya 16 bora ndani ya dimba la Parc des Princes?

Zawadi ya penati waliyopewa Man United kufuatia mpira uliopigwa na Diogo Dalot kugonga mkono wa Kimpende ilitosha kuwafanya washinde bao muhimu na kuwatoa PSG kitu ambacho dunia nzima hawakuamini.

Kuna mitazamo ya aina mbili tofauti kuhusu VAR. Mosi ni kwamba watu wanakubaliana kwa kauli moja kwamba teknolojia hiyo imekuja na inatenda haki kwenye matukio mbalimbali ambayo hapo kabla yalikuwa siyo rahisi kuonekana na waamuzi.

Mtazamo wa pili ni kwamba wadau wanadai VAR imekuja kupunguza umakini wa waamuzi uwanjani na wakati mwingine wanafanya maamuzi siyo sahihi kitu ambacho kinapunguzu ladha ya mchezo.

Tofauti na ilivyokuwa kwenye ligi ya mabingwa ulaya, Bundesliga na La Liga ambao walianza kutumia teknolojia hiyo tangu msimu uliopita. Ligi ya Uingereza wao wameanza kutumia teknolojia hiyo msimu huu.

Hadi kufikia sasa kwenye mzunguko wa 12 teknolojia hiyo imeshafanya kazi na kuingia kwenye matukio mengi sana na kutoa uamuzi mbalimbali.

Makala haya ya SportPesa News yanakuangazia matukio matano makubwa yaliyoingiliwa na kutolewa uamuzi na VAR msimu huu.

NB: Katika matukio haya yapo ambayo yalifanyiwa uamuzi ambao ni sahihi na baadhi yaliotolewa uamuzi ambao umeonesha kuna utata.

Manchester City 2-2 Tottenham Hotspurs

Mechi hii ilikuwa ni kwenye mzunguko wa pili ambapo ndani ya dimba la Etihad, Man Cirty walikuwa wakiwakaribisha Tottenham Hotspurs. Hiyo ilikuwa ni Agosti 17.

Baada ya piga nikupige timu hizo zilifika kwenye dakika za majeruhi matokeo yakiwa ni 2-2. Kwenye sekunde za mwisho kabisa Man City walihisi kunyakuwa alama zote tatu baada ya Gabriel Jesus kuukwamisha mpira wavuni.

Wakati wachezaji wa Man City pamoja na watu wao wa benchi la ufundi sambamba na mashabiki wakiwa kwenye dimbwi zito la furaha ndipo mwamuzi Michael Oliver alitonywa kuhusu tukio fulani kabla ya bao kufungwa.

Mwamuzi aliambiwa kuwa Aymeric Laporte ambaye ni mlinzi wa Man City aliunawa mpira kabla ya kufika kwa mfungaji na hivyo baada ya kuhakikishiwa kuhusu suala hilo alilifuta bao hilo na mechi ikaisha kwa 2-2.

Hilo ndiyo lilikuwa tukio la kwanza kubwa zaidi la kusisimua msimu huu ambapo mashabiki wa soka la Uingereza walianza kulishuhudia.

Hata hivyo kwenye tukio hilo uamuzi ulikuwa ni sahihi hasa ukizingatia sheria mpya za kuunawa mpira ndani ya boksi.

Arsenal 2-2 Crystal Palace

Mechi ya Novemba 2 ambapo Arsenal walikuwa nyumbani kuilika Crystal Palace. Kwenye wiki hii naweza kusema kuwa EPL ilishuhudia matukio mengi sana yakiamuliwa na VAR.

Ndani ya mechi hii tu Crystal Palace walizawadiwa penati ambayo ilitokana na VAR. Lakini tukio kubwa zaidi ilikuwa ni kwenye dakika za majeruhi ambapo mlinzi wa Arsenal, Sokratis Papastathipoulos alidhani kuwa amefanikiwa kuipa timu yake bao la tatu na ushindi kwenye mchezo huo.

Bao hilo alifunga kwa kichwa na baada ya kushangilia kwa muda mrefu mwamuzi alilifuta bao hilo kwa madai kuwa mchezaji wa Arsenal, Collum Chambers alimfanyia madhambi Gary Cahil wa Palace kabla ya kufungwa kwa bao hilo hivyo bao likafutwa na mechi ikaisha 2-2.

Maamuzi hayo yalikuwa na utata hasa ukiangalia kwa umakini madhambi aliyochezewa Cahil dhidi ya Chambers

Liverpool 3-1 Manchester City 

Mechi ya Novemba 10 ambayo nayo imeacha maswali mengi hadi hivi sasa. Mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya wapinzani wawili kwenye mbio za ubingwa tumeshuhudia mwamuzi Michael Oliver akishindwa kuomba usaidizi wa VAR licha ya kuwa ilionekana dhahiri kulikuwa na matukio hasi.

Tukio kubwa kabisa ni la mlinzi wa pembeni wa Liverpool, Alexander Anorld kuonekana kuushika mpira ndani ya boksi akijaribu kuzuia krosi iliyopigwa na Raheem Sterling.

Ukiangalia aina ya penati ambazo zimekuwa zitolewa kwa timu mbalimbali tangu VAR ilipoanza kufanya kazi huwezi kuona ni namna gani City wangenyimwa penati.

Hata hivyo Oliver hakuona na hata watu waliokuwa kwenye monitors za VAR hawakutaka kuangalia licha ya kuwa kocha Pep Guardiola pamoja na wachezaji wake kulalamikia sana tukio hilo.

Tottenham Hotspurs 1-1 Shefield United 

Mechi ya Novemba 10 ambayo iliwakutanisha wenyeji Spurs dhidi ya Shefield United. Mechi hiyo iliisha kwa timu hizo kufungana bao 1-1.

Hata hivyo Shefield wanahisi pengine wangepata alama zote tatu kama siyo bao lao kukataliwa kwa utata kutokana na madai ya mchezaji wao kuotea.

Mshambuliaji wao David McGoldrick alifunga bao safi lakini kwa mujibu wa VAR ni kwamba wakati wa kutengeneza bao hilo, Enda Steven alikuwa wakati akipokea pasi ambayo nayo aliipiga kati na kwenda kuzaa bao.

Hata hivyo picha nyingi za marudio zinaashiria utata mwingi ukigubika tukio hilo kwani mistari iliyopigwa wakati wa kuangalia haioneshi kama ni kweli Enda alikuwa ameotea bali inaonesha Eric Dier ambaye ni mlinzi wa Spurs kuwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kabisa.

Brighton 3-2 Everton

Wakati zikiwa zimesalia dakika 10 mpira kuisha, Everton walikuwa mbele kwa bao 2-1. Mchezo huo ulikuwa ni Oktoba 26.

Kwenye dakika ya 80, kupita VAR, Brighton wakazawadiwa penati kwa madai kuwa Michael Keana alimgonga mshambuliaji wa Aaron Connolly kwa nyuma.

Hata hivyo picha za marudio hazikuwa zikionesha madai hayo na ni kwambie tu kuwa hili ni moja kati ya matukio ambayo yameombewa radhi.

FA kupitia kitengo chake cha VAR wamekuwa na kawaida ya kupitia matukio mbalimbali na kisha kuyatolea ufafanuzi.  

Kwenye tukio la penati ya Brighton kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa mara baada ya mchezo huo ni kwamba Everton walionewa.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya