AFCON 2021: Nyota Hawa Wa Simba Na Yanga Vibaruani Leo. Fuatilia Dondoo

14th November 2019

MAPUTO, Msumbiji- Mshambuliaji hatari wa klabu ya Simba na kinara wa mabao ligi kuu bara Meddie Kagere pamoja na winga mpya wa Yanga, Patrick Sibomana leo majira ya saa moja usiku wanashuka uwanjani na timu yao ya taifa Rwanda

Meddie Kagere
Meddie Kagere
SUMMARY

Rwanda wao kwenye mechi zao tano za mwisho wameshinda mara tatu ikiwemo ushindi wa 7-0 dhidi ya Shelisheli na wamekwenda sare mara mbili. Ikiwa na maaana kwamba hawajafungwa kwenye mechi tano za mwisho.

MAPUTO, Msumbiji - Mshambuliaji hatari wa klabu ya Simba na kinara wa mabao ligi kuu bara Meddie Kagere pamoja na winga mpya wa Yanga, Patrick Sibomana leo majira ya saa moja usiku wanashuka uwanjani na timu yao ya taifa Rwanda ili kukabliana na Msumbuji ambao watakuwa nyumbani.

Mchezo huo ni wa kundi F kugombea tiketi ya kufuzu michuano ya Afcon ambayo imepangwa kufanyika mwaka 2021 nchini Cameroon.

Rwanda na Msumbuji zote hazikufanikiwa kufuzu kwenye Afcon iliyopita lakini sasa timu moja wapo inaweza kupata nafasi kupitia kundi hili ambapo pia wenyeji Cameroon wamo ndani yake.

Cameroon wao ingawa wamepangwa kwenye hatua ya makundi lakini tayari wameshafuzu moja kwa moja bila kujali nafasi watakayomalizia hivyo ni kazi kwa timu tatu zilizobaki kugombea nafasi mbili.

Kwenye kundi hilo pia wamo Cape Verde ambao jana wakiwa uginini wametoka sare tasa na Cameroon.

Mchezo wa leo baina ya Rwanda na Msumbuji ni mgumu kwa pande zote mbili hasa ukizingatia fomu zao za hivi karibuni.

Msumbuji kwenye michezo yao mitano iliyopita wameshinda mechi nne dhidi ya Kenya, Mauritius, Mauritius tena, na Madagascar huku kipigo chao cha mwisho walifungwa 1-0 na Madagascar Julai 28, mwaka huu.

Rwanda wao kwenye mechi zao tano za mwisho wameshinda mara tatu ikiwemo ushindi wa 7-0 dhidi ya Shelisheli na wamekwenda sare mara mbili. Ikiwa na maaana kwamba hawajafungwa kwenye mechi tano za mwisho.

Timu hizo zinakutana leo ikiwa ni mara yao ya tatu. Mara ya kwanza kabisa walikutana mwaka 2015 ambapo Rwanda walishinda 1-0 kwenye mchezo wa ugenini na kwenye mechi ya marudiano iliyofanyika mwaka 2016, Msumbuji walishinda 3-2 na kusonga mbele.

Nyota wa Yanga, Patrick Sibomana akiwa na moto baada ya kutoka kufunga bao muhimu kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Ndanda atakuwa na nia ya kuendeleza fomu yake hiyo nzuri ingawa amekuwa hana nafasi ya uhakika ndani ya kikosi hicho cha Amavubi.

Kagere ambaye ndiyo mshambuliaji tegemezi wa timu hiyo kama ilivyo kwenye klabu yake ya Simba atakuwa akiongoza mashambulizi akiwa kama mchezaji wa ushambuliaji wa kati.

Shikalo v Misri

Mechi nyingine leo itakuwa ni ile ya kundi G ambapo majirani zetu Kenya watakuwa kwenye jiji la Cairo nchini Misri kuoneshana kazi dhidi ya wenyeji hao.

Kwenye kikosi cha Kenya yupo kipa namba moja wa Yanga, Farouk Shikalo ambaye hata na hivyo hajajihakikishia namba mbele ya Patrick Matasi ambaye kwasasa anacheza klabu ya St George ya Ethiopia.

Hata hivyo ni jambo la kusubiri na kuona kama kocha Francis Kamanzi atamuamini Shikalo ambaye kwa hivi sasa amekuwa akionesha kiwango kizuri akiwa na timu yake ya Yanga.

Misri watambulika kuwa ni moja kati ya timu bora sana barani Afrika tofauti na Kenya ambao hawana historia kubwa. Kwenye Afcon iliyopota iliyofanyika nchini Misri, Kenya nao walipata nafasi ya kushiriki.

Mchezaji anayetegemewa zaidi kwa Kenya ni kiungo wa Tottenham Hotspurs, Victor Wanyama. Kwa upande wa Misri kuna nyota wengi sana lakini kwa leo watakosa huduma ya Mohamed Salah ambaye ni majeruhi.

Kwenye historia timu hizi zimekutana mara moja hiyo ikiwa ni mwaka 2014 ambapo Misri walishinda kwa bao 1-0.

Kenya hawajashinda mchezo hata mmoja kwenye mechi zao tano za mwisho walizocheza huku Misri wakiwa wameshinda mechi nne na kufungwa mchezo mmoja.

Ghana v Afrika Kusini

Macho na masikio ya wapenda soka wa bara la Afrika yataelekezwa kwa wingi nchini Ghana ambapo majira ya saa nne usiku watawakaribisha Afrika Kusini.

Ingawa timu hizo zimekuwa na historia safi ya ukubwa wa soka lao lakini naweza kusema kuwa wamekuwa na bahati mbaya sana hasa kwenye michuano ya Afco.

Afrika Kusini wamekuwa ni moja ya nchi ambayo imekuza sana mpira Afrika na wengine wamekuwa wakiitaja kama Ulaya ndogo. Lakini cha ajabu ni kwamba wamekuwa wanashindwa hata kufuzu Afcon wakati mwingine.

Nao Ghana licha ya kuwa na nyota wengi wanaosakata soka Ulaya lakini bado wanasaka nafasi ya kubeba taji hilo kama ilivyo kwa vigogo wengine kama Senegal.

Mechi ya leo itakuwa safi kwa mpira wa ufundi mwingi na kushambuliana na ndiyo maana SportPesa tulidokeza tangu jana kwamba hii siyo mechi ya kuikosa.

Tangu mwaka 2002 timu hizo zimekutana mara tano. Matokeo ya mechi hizo ni kwamba wametoka sare mara nne na mechi moja Ghana walishinda kwa 2-1 hiyo ilikuwa ni mwaka 2015.

Mechi zao tano za mwisho Afrika Kusini wamefungwa mara 3 na wameshinda mara mbili ukiwemo ushindi wa 1-0 dhidi ya Misri ambapo walifanikiwa kuwaondosha wenyeji kwenye Afcon.

Wao Ghana kwenye mechi zao tano za mwisho wameshinda mara moja, sare mara mbili na wamefungwa mara mbili.

Mechi Nyingine: 

Mali v Guinea

Ghana v Afrika Kusini

Angola v Gambia

DR Congo v Gabon

Msumbiji v Rwanda

Misri v Kenya

Togo v Comoros

Algeria v Zambia

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya