AFCON 2021: Kaseja Atetea Kiwango Cha Mbwana Samatta Stars Mechi Dhidi Ya Libya

21st November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania -Siku mbili baada ya timu ya taifa ya Tanzania "Taifa Stars" kupoteza kwenye mchezo wake wa kundi J kwa kufungwa 2-1 dhidi ya Libya, mlinda lango mkongwe wa timu hiyo Juma Kaseja ameibuka na kumkingia kifua Mbwana Samatta

Juma Kaseja na Mbwana Samatta
Juma Kaseja na Mbwana Samatta
SUMMARY

"Siyo jambo zuri kumtupia lawama mchezaji mmoja, tumefungwa wote kama timu lakini ukitoa michezo hii iliyopita nadhani shughuli ya Samatta huwa tunaiona kwenye kulipambania taifa lake, ni mchezaji muhimu na wachezaji wote kwenye kikosi tunalijua hilo," amesema Kaseja.

DAR ES SALAAM, Tanzania -Siku mbili baada ya timu ya taifa ya Tanzania "Taifa Stars" kupoteza kwenye mchezo wake wa kundi J kwa kufungwa 2-1 dhidi ya Libya, mlinda lango mkongwe wa timu hiyo Juma Kaseja ameibuka na kumkingia kifua Mbwana Samatta kutokana na lawama anazotupiwa.

Mahabiki wengi wa soka hasa kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakihoji kuhusu uwezo alioonesha Samatta kwenye mechi mbili zilizopita dhidi ya Equatoria Guinea ambao Stars walishinda 2-1 nyumbani na ule uliopita dhidi ya Libya.

Wengi wao wanadhani kwamba Samatta hajitumi ipasavyo kwenye timu ya taifa kama anavyofanya akiwa na klabu yake ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji ambayo hivi sasa inashiriki ligi ya mabingwa ulaya.

Hata hivyo Kaseja amesema siyo kweli kwamba Samatta hajitumi bali ni kitu cha kawaida kwa mchezaji kufshindwa kufanya vyema kwenye baadhi ya michezo anayokabiliana nayo.

"Siyo jambo zuri kumtupia lawama mchezaji mmoja, tumefungwa wote kama timu lakini ukitoa michezo hii iliyopita nadhani shughuli ya Samatta huwa tunaiona kwenye kulipambania taifa lake, ni mchezaji muhimu na wachezaji wote kwenye kikosi tunalijua hilo," amesema Kaseja.

Tumetekeleza Mpango Wa Kocha

Kaseja amefafanua kuhusu aina ya mchezo waliocheza hasa kipindi cha pili ambapo walionekana kuzidiwa na amesema kuwa ule ulikuwa ni mpango wa mwalimu lakini kwa bahati mbaya haukutimia.

"Kila kocha huwa ana mpango wake kwenye mchezo husika, kwenye mechi ile mwalimu alituelekeza kitu cha kufanya na sisi tulijitahidi kutekeleza lakini kwa bahati mbaya tumefungwa kwahiyo ni hali tu ya mchezo na tutajipanga zaidi kwenye michezo ijayo," amesema Kaseja.

Kikosi cha Stars kimeingia nchini usiku wa kuamkia leo wakitokea Tunisia ambapo siku ya Jumanne walicheza mechi ya pili ya kundi J dhidi ya Libya. Mchezo huo uliisha kwa Stars kufungwa mabao 2-1 huku bao la Stars likufungwa na Samatta kwa njia ya mkwaju wa penati.

Msimamo wa kundi unaonesha kuwa Tunisia baada ya kushinda mechi zake zote mbili anaongoza akiwa na alama 6 huku Libya wenye alama 3 wakiwa kwenye nafasi ya pili sawa na Stars wenye alama 3 kwenye nafasi ya 3. Guinea wanaburuza mkia wakia hawana alama.

Mechi ijayo ya makundi kufuzu Afcon Stars watacheza ugenini dhidi ya Tunisia, Agosti 31, 2020.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya