AFCON 2021: Hivi Ndivyo Ilivyokuwa Safari Ya Stars Kufuzu Afcon Ya 2019

14th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Siku ya Ijumaa majira ya saa moja usiku timu ya taifa ya Tanzania itashuka kwenye uwanja wa taifa kukabiliana na Equatorial Guinea

Simon Msuva
Simon Msuva
SUMMARY

Usiku wa Machi 24, 2018, utabaki kwenye kumbukumbu za Watanzania wengi wapenda soka baada ya kushuhudia timu yao ya taifa ikiichapa Uganda mabao 3-0 uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kufuzu fainali za Afconi 2019.

DAR ES SALAAM, Tanzania- Siku ya Ijumaa majira ya saa moja usiku timu ya taifa ya Tanzania itashuka kwenye uwanja wa taifa kukabiliana na Equatorial Guinea mchezo wa kundi J kuwania kufuzu michuano ya Afcon itakayofanyika nchini Cameroon mwaka 2021.

Kwenye kundi hilo timu nyingine ni Tunisia na Libya ambapo kama Stars watafanikuwa kumaliza kwenye nafasi mbili za juu basi watakuwa wameweka rekodi ya kushiriki michuano hiyo mara mbili mfululizo.

Iliwabidi Stars wasubiri kwa miaka 39 hadi kufanikiwa kufuzu kucheza Afcon ya Misri iliyofanyika katikati ya mwaka huu.

Safari ya kufuzu kwenye Afcon ya Misri haikuwa rahisi hata kidogo kama watu wanavyodhania lakini jitihada za mwalimu Emmanuel Amunike pamoja na wachezaji zilituwezesha kufuzu tukitukokea kundi L ambapo ndani tulikuwa Uganda, Lesotho, Cape Verde.

Wakati tunajiandaa kuinza safari mpya ya kusaka tiketi yetu nyingine, siyo vibaya kama tukajikumbusha safari yetu iliyopita hadi kufuzu ilikuwaje.

Tanzania 1-1 Lesotho

Safari ya Tanzania kufuzu fainali za Afcon 2019 zilianza kwa dosari baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Lesotho tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani ambapo mechi hii ilipigwa Chamazi Complex, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilichezwa Juni 10, 2017 ambapo kocha wa Stars alikuwa ni Salum Mayanga na walianza kupata bao la mapema dakika ya 27 kupitia kwa Nahodha wake, Mbwana Samatta kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuangushwa nje ya boksi. 

Hata hivyo, bao hilo halikudumu, kwani Lesotho walisawazisha dakika ya 34 kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi ya Jane Thaba-Ntso.

Uganda 0-0 Tanzania

Septemba 8, 2018 Taifa Stars walisafiri kuwafuata Uganda ukiwa ni mchezo wa pili kwa timu zote mbili. Kwenye uwanja wa Nambole Kampala.

Kwenye mechi hii tayari Stars walikuwa na kocha mwingine ambaye ni Emmanuel Amunike aliyemrithi Mayanga. Mechi hiyo iliisha kwa suluhu tasa na kuwafanya Stars kufikisha alama 2 kwenye msimamo wa kundi L.

Stars wangeweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kama nahodha Samatta angeitumia nafasi nzuri zaidi waliyoipata kwenye mchezo huo ambapo alibaki ana kwa na mlinda lango wa Uganda, Denis Onyango lakini alishindwa kufunga.

Cape Verde 3-0 Tanzania

Matumaini ya Watanzania kuishuhudia timu yao Taifa Stars ikifuzu Afcon ya 2019 yalififia Oktoba 12, 2018 baada ya kuishuhudia timu hiyo ikipokea kichapo cha mabao 3-0 na wenyeji, Cape Verde. 

Pambano hilo lilichezwa kwenye uwanja wa Nacional de Cabo Verde uliopo mji kuu wa Praia. Katika mchezo huo mabao ya wenyeji yalifungwa na Ricardo Jorge Pires Gomes aliyefunga mawili na beki Ianique dos Santos Tavares Stopira.

Tanzania 2-0 Cape Verde

Wachezaji wa Taifa Stars baada ya kujiuliza kufuatia kipigo cha mjini Praia, Oktoba 16, 2018 waliweza kuwapoza machungu na kurudisha matumaini ya kufuzu fainali hizo baada ya kuifunga Cape Verde mabao 2-0, huo ukiwa ni mchezo wa marudiano uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mabao ya Stars katika mechi hiyo yalifungwa na Simon Msuva dakika ya 29 na Mbwana Samatta dakika ya 58 na siku ya pili Rais aliita timu Ikulu na kuwapongeza kwa kulipiza kisasi na kuwachangia 50 Milioni kwa ajili ya mechi mbili zilizobakia dhidi ya Lesotho ambayo wangecheza ugenini na Uganda.

Lesotho 1-0 Tanzania

Novemba 18, 2018, ilikuwa siku mbaya kwa wachezaji wa Taifa Stars wa wakati huo pamoja na viongozi wa Shirikisho la soka TFF, baada ya timu hiyo kupoteza mchezo muhimu kwa kufungwa bao 1-0 na wenyeji, Lesotho.

Bao pekee la beki wa klabu ya Matlama, Nkau Lerotholi dakika ya 76 lilitia kiza safari ya Stars kuelekea Misri na sasa kulazimika kusubiri mechi ya mwisho kati yake na Uganda kwani yeye na Lesotho walikuwa wanalingana kwa pointi wote wakiwa na alama tano.

Tanzania 3-0 Uganda

Usiku wa Machi 24, 2018, utabaki kwenye kumbukumbu za Watanzania wengi wapenda soka baada ya kushuhudia timu yao ya taifa ikiichapa Uganda mabao 3-0 uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kufuzu fainali za Afconi 2019.

Ushindi tu ulikuwa hautoshi kuwafanya Stars wafuzu Afcon bali matokeo ya mechi kati ya Lesttho dhidi ya Cape Verde ndiyo yalikuwa yakifuatiliwa takribani nchi nzima. Kama Lesotho wangeshinda basi hata Stars wangeshinda bao ngapi isingesaidia.

Kwa bahati nzuri Cape Verde waliwalazimisha sare Lesotho na hivyo Stars ikaandika historia mpya baada ya miaka 39 kupita.

Katika mchezo huo mabao ya Stars, yalifungwa na Simon Msuva dakika ya 21, Erasto Nyoni aliyefunga kwa penalti dakika ya 51 na Aggrey Morris dakika ya 57.

Kwa ushindi huo, Taifa Stars iliungana na Uganda kufuzu AFCON kama mshindi wa pili wa kundi L ikifikisha pointi nane, nyuma ya Uganda iliyomaliza na pointi 13 na kuziacha Lesotho iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi sita na Cape Verde pointi tano.

Imeandaliwa na Raheem Mohamed